Jaji Nsekela: Kiongozi wa Umma kuwa tajiri sio dhambi



Mhe. Jaji (Mst.) Harold Nsekela, Kamishna wa Maasili, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 haimkatazi mtu yeyote kuwa tajiri kama ameupata utajiri huo kwa mujibu wa Sheria.



Kamishna Nsekela amesema hayo hivi karibuni Jijini Mbeya katika mafunzo ya Maadili kwa viongozi wa umma wa mkoa wa Mbeya, mafunzo hayo yamefanyika
katika ukumbi wa Benjamini Mkapa jijini humo.



“Katiba haikatazi wewe kuwa tajiri, haikatazi mimi kuwa tajiri, lakini huo utajiri wako uupate kwa mujibu wa sheria,” amesema na kuongeza kuwa, “utajiri sio
dhambi sio kosa, kinachokatazwa ni kwamba utajiri wako uupate kwa mujibu wa sheria.”



Amesema kuwa wapo baadhi ya viongozi wa umma wanaoogopa kujaza fomu za Tamko la Raslimali na Madeni, wakati kujaza fomu hizo ni takwa la Kikatiba na Kisheria.



“Najua ni kero kwa maana ya kwamba hatulipendi. Kama umepata mali zako kihalali unaogopa nini kujaza tamko. Kama unaona kujaza tamko ni kero, kwanini unalipa kodi, kwani kulipa kodi sio kero, nani anataka kulipa kodi si wote hatutaki, ameuliza Kamishna Nsekela.



Alisema kuwa, ni lazima mjaze tamko la rasilimali na madeni pamoja na kuwa baadhi ya viongozi wa umma hatulipendi kulijaza tamko hili, tunajiuliza kwanini
tuulizwe mali tulizonazo?



“Kujaza tamko la raslimali na madeni unaogopa nini? Kama una mawazo potofu kwamba kujaza tamko ni kero kwanini unalipa kodi, kwani kulipa kodi sio kero,” aliuliza. Na kuongeza kuwa, “ Ndio maana Serikali ikaweka mfumo wa ulipaji kodi kwa watumishi wa umma haikungoji kulipa kodi wanakata mshahara wako huko huko.”



Alisema kuwa kama kuna kiongozi ambaye hadi sasa hajajaza tamko kwa mujibu wa sheria, ajaze haraka na atoe sababu kwa nini amechelewa kujaza tamko hilo.



“Wale wote ambao hawajajaza wajaze, wajaze haraka na watoe sababu. Agizo hili ni kwa viongozi wote Tanzania nzima sio Kanda za Juu Kusini peke yake.”



Jumla ya viongozi 45 wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini hawakujaza Tamko la Raslimali na Madeni ilipofika tarehe 31Desemba, 2019 kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995.



Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Albert Chalamila alisema zana ya maadili ni zana nzuri sana kwasababu inamfanya kila kiongozi kujipima mwenendo wake.



“Uadilifu unamtaka kila kiongozi kutawala cheo chake ili asisimamiwe na mtu mwingine. Lakini maadili sio lazima uwe maskini, lakini uwe muwazi katika upatikanaji wa mali ulizo nazo.”



Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa wa Mbeya, kiongozi wa umma akitumia ndivyo sivyo madaraka yake kwa kujaza kiapo cha Ahadi ya Uadilifu na kushindwa kukitmiza hayo ni matumizi mabaya ya madaraka.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad