Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema yanayotokea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa si kitu kipya, na kwamba hakuna chama ambacho hakina vuguvugu kama ilivyo kwa chama hicho.
Jaji Warioba aliyasema hayo wakati akihojiwa katika kipindi cha Konani kinachorushwa na Televisheni ya ITV ambapo alitakiwa kutoa maoni yake kutokana na yanayoendelea ndani ya CCM ya kuwahoji wanachama wake.
Kamati ya Maadili ya chama mwishoni mwa wiki iliwaita wanachama wake watatu kuwahoji ambao ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bernard Membe na waliokuwa makatibu wakuu wa chama hicho, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana.
Jaji Warioba alisema si kitu kipya kwa chama hicho kwa kilichotokea na kwamba hakuna chama ambacho hakina vuguvugu. Akizungumza kuhusu Katiba Mpya, Warioba katika mchakato huo alisema haiwezi kuzuiliwa kwa sababu ya gharama.
“Tume ya Katiba Mpya ilichukua maoni nchi nzima ilikuwa ni gharama, lakini zinafaida zake kwa sababu tunajua maoni ya wananchi na yapo yametunzwa.
“Bunge Maalum la Katiba lilikuwa na gharama, lakini lilikamilika, gharama iliyobaki ni kupata kura za maoni.
“Nitastaajabu kama mnataka uchaguzi na kura ya maoni ni uchaguzi ikiwa mtachagua viongozi ni sawa, lakini wananchi wakitaka kutunga Katiba yao siyo sawa, mnasema gharama, hii siielewi.”
Katika mahojiano hayo Jaji Warioba alisema hata uchaguzi gharama zake ni kubwa, na kufafanua kuwa katiba ndiyo moyo wa taifa, na kwamba haiwezi kuzuilika.
“Kwa kusema hivyo, yapo mambo mengi utayaacha sioni kama ni gharama kubwa sana… huko nyuma tulizitengeneza zilikuwa na gharama mfano ni Katiba ya mwaka 1977 ilikuwa na gharama, mambo ya maendeleo ni gharama, lazima tuyakubali,” alisema.
Akizungumzia Katiba iliyopo, Jaji Warioba alisema ina afya, na kwamba Katiba Mpya kazi yake ni kuboresha yaliyopo.
Hata hivyo, alisema Katiba Mpya utangulizi wake ni mzito zaidi ambao unaonyesha dhamira ya kuitunga na katika sura ya nne na ya tano imefafanua madaraka ya wananchi.
“Imefafanua zaidi kuwa Katiba ni Sheria Kuu, pia imeingiza umuhimu wa utamaduni wa kitaifa ndiyo maana ya tunu, imefafanua kwa upana zaidi malengo ya nchi inakoelekea, imeweka misingi ya uongozi na miiko ya uongozi na haki za binadamu na uraia,” alisema.