Muasisi wa muziki wa kitamaduni wa Zulu wa Afrika Kusini, Joseph Shabalala amefariki dunia februari 11, 2020 akiwa na umri wa miaka 78 ambapo katika tasnia ya muziki alisaidia kuutambulisha vyema muziki wa kitamaduni wa Kizulu ulimwenguni Shabalala alizaliwa mwaka 1941.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa meneja wa bendi ya Ladysmith Black Mambozo imesema kuwa Shabalala amefariki dunia katika hospitali ya mjini Pretoria nchini Afrika Kusini, Taarifa hiyo haijabainisha ugonjwa uliopelekea umauti wa Shabalala.
Mwanamuziki huyo alifahamika zaidi kama muasisi na muongozaji wa kikundi cha kwaya cha Ladysmith Black Mambazo, kilichoshinda tuzo tano za Grammy, alikianzisha kikundi hicho mwaka 1964.
Walipata umaarufu duniani baada ya kupewa kazi ya kuimba katika albamu iliyouzwa mamilioni ya pesa ya Paul Simon iliyojulikana kama Graceland, hasa katika wimbo wao wa Homeless, wimbo ulioandikwa na Shabalala akishirikiana na Simon.
Katika muda wake wa ziada alipendelea kuimba na rafiki zake, baadaye alikuwa kiongozi na mtunzi mkuu wa kwaya ambaye alijikita katika nyimbo za Zulu ambazo mara nyingi ulikuwa na muziki laini na dansi ya kuvutia.
Shabalala alistaafu kucheza katika matamasha mwaka 2014 muda mfupi baada ya kucheza katika tamasha lililoandaliwa kwa ajili ya Nelson Mandela.
Mbali na muziki, marehemu enzi za uhai wake alitamba pia kwenye filamu na baadhi ya kazi zake ni pamoja na ‘On Tiptoe’ na ‘Gentle Steps to Freedom’.