Kenya: Hatua zilizochukuliwa na Shirika la Feri Baada ya Mama na Mwana Kufa Maji
0
February 18, 2020
Miezi minne iliyopita shirika la feri la Kenya lilishutumiwa vikali wakati Mariam Kigenda na mwanae wa miaka minne Amanda Mutheu walipotumbukia baharini wakafa maji wakiwa kwenye gari lao katika kivuko cha Likoni mjini Mombasa pwani ya Kenya.
Je, tangu mkasa huo shirika hilo la feri limechukua tahadhari gani kuona kwamba kuna usalama katika kivuko hicho cha Likoni? Nimekua huko nijionee mwenyewe hali ilivyo.
Unapofika hapo kuna mtangazaji anayekumbusha abiria kuhusu usalama wao wakiwa kwenye feri:`` Kumbuka kushusha vioo ukiwa ndani na feri na ufungue mkanda wako, na ukiweza utoke nje,'' anasema mtangazaji huyo kupitia kipaza sauti.
Ndani ya feri ya MV Kilindini, mkurugenzi mkuu Bakari Gowa anaeleza ni hatua zipi walizochukua kuwahakikishia watuamiaji wa feri hiyo usalama wao..
Gowa anaeleza kuhusu kanuni ya magari kuegeshwa ndani mwa feri:`` Hii ni sehemu ambayo ni kama mita sita hadi nane halafu kuna sehemu ya ramp umbali wa mita sita, kwa jumla kuna umbali wa mita kumi na mbili kutoka kwa mlango wa feri na hapa magari yameegeshwa.''
BBC ilimuuliza Gowa kwanini wenye magari hawatoki nje maana yake mama na mwanae walipozama, wakenya wengine walilaumu shirika hilo kwa kutotilia mkazo amri kwa abiria kutoka nje ya magari yao. Gari la mama huyo ndilo lilikua limeegeshwa mwisho kabisa lilipotumbukia baharini.
``Si lazima abiria watoke nje ya magari yao,'' anasema Gowa, ``ukiangalia kivuko cha Likoni si kirefu sana. Feri huchukua kama dakika saba hivi zifike upande huo mwingine. Muda ni kidogo sana. Kila mtu akianza kutoka kwenye gari lake huku wengine wana watoto kisha tena feri ikifika waanze kuingia kwenye magari yao haitawezekana maanake feri ikifika hivi kuna wengine wanajitayarisha kuingia. Isitoshe feri zetu zingine hazina nafasi ya abiria kusimama akitoka nje.
``Tumechunguza hali hii ya usalama tukaona wako sawa. Tunalosisitiza ni kila mtu ashushe vioo vya magari, wazime gari pia na kufungua mikanda. Hii inatusaidia kujua idadi ya watu waliomo kwenye kila gari. Na kuna watu wetu hapa kama yule unamuona kazi yake ni kukumbusha watu washushe vioo na kufungua mikanda yao. Hizo ni kanuni lazima zifuatwe. Kama abiria hawezi kushusha vioo vya gari lake itabidi ashuke nje ya gari hilo.''
Kuhusu masuala ya usalama Gowa anazungumza kuhusu mipango ya kuwa na boti la uokoaji:
``Hiyo mipango tunayo, la muhimu ni pesa zikipatikana tutatekeleza hilo maana yake ni muhimu tuwe na watu wa kuokoa maisha hapo na boti lao kila siku, mchana na usiku wakifanya kazi kwa zamu. Hii itatuwezesha kuokoa abiria akipatwa na mkasa. Na pia kuna wale hujirusha baharini wenyewe kutokana na matatizo yao binafsi. Hatuwezi kuwaacha hata kama wamejirusha wenyewe. Nao pia lazima waokolewe.''
Baadhi ya watumiaji wa feri wanasema wameridhishwa na juhudi za shirika la feri la Kenya kuhusu usalama wao wanapotumia kivuko hicho cha Likoni, na wanahimiza shirika hilo liwe na wapiga mbizi wa kuokoa maisha hapo Likoni kila siku.
Tags