Kinana, Makamba Wana Jambo..Kiza Kinene



KIZA kinene kimetawala kuhusu kuhojiwa kwa makatibu wakuu wawili wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana.

Hadi kufikia jana, si Kinana wala Makamba aliyefika kuhojiwa na Kamati ya Maadili na Nidhamu ya CCM tofauti na kauli ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula anayeongoza kamati hiyo, kwamba makada wake wote watatu waliotakiwa kuhojiwa kwa makosa mbalimbali ya kimaadili wengehojiwa ndani ya wiki hii.

Hadi sasa kamati hiyo imemuhoji Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani, Bernard Membe ambaye aliwekwa kwenye kundi moja la kuhojiwa na Kinana na Makamba.
Kushindwa kufika huko kwa Kinana na Makamba kuliibua taarifa nyingine mpya jana kwamba viongozi hao wastaafu wamegoma kufika kuhojiwa.
Uamuzi wa kutaka makada hao wahojiwe ulifikiwa Desemba 13 mwaka jana, baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kuketi na kuagiza waitwe baada ya kutuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya kimaadili, msingi ukiwa ni mgogoro kati yao na chama hicho pamoja na mwenyekiti wao.

Taarifa ambazo zinaeleza kuwa Kinana na Makamba ambao inasemekana kwamba wote wako nchini, wamegoma kuhojiwa kwa kile ambacho kinaelezwa hawako tayari kudhalilishwa.

Inaelezwa kuwa hoja kubwa ni kwamba hawawezi kuhojiwa ama kudhalilishwa na watu ambao wameingia CCM juzi juzi.

Kwamba watakuwa tayari kuzungumza iwapo kitaitwa kikao kitakachowahusisha viongozi wakuu wa zamani, wakiwamo wenyeviti na makamu wenyeviti wastaafu wa chama hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, ingawa hawajaandika barua ya kuondoka CCM, inaelezwa kama ikibidi watafanya hivyo na hasa ikiwa kikao hicho cha viongozi wastaafu hakitaitwa.

Alipo pigiwa simu mzee Makamba ambapo licha ya kusema kuwa yupo Lushoto mkoani Tanga, lakini alikataa kuzungumza chochote kuhusu kuhojiwa kwake.
Tofauti na kauli yake ya siku za nyuma kwamba akiitwa atafurahi na atakuwa tayari kwenda kuhojiwa, jana Makamba alionekana kuwa mkali kidogo huku akiongea kwa hamaki.
“Nimekwambia mimi sina shida na waandishi kwa sasa, mimi nipo Lushoto huku, hizo habari sizitaki, kama nitakuwa nina shida ya waandishi nitawatafuta mwenyewe, kwa sasa andikeni habari za mvua,” alisema Makamba.

Mwandishi alipomuuliza iwapo kama mvua hizo ndizo zilizomzuia kutofika Dodoma kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu na Maadili au amekataa kuhojiwa kama taarifa nyingine zinavyoeleza, alijibu; “Nimesema sitaki waandishi kwa sasa, niacheni nipumzike.”
Juhudi za kumpata Kinana ziligonga mwamba


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad