Kusambaa kwa virusi vya Corona imekuwa ni janga kwa soka Italia baada ya mechi tano za Serie A ikiwamo ya Juventus dhidi ya Inter Milan zitachezwa bila ya mashabiki.
Mechi nyingine ni zile za Udinese, AC Milan, Parma na Sassuolo zote zitachezwa bila ya mashabiki.
Michezo ya Lazio, Napoli, Lecce na Cagliari yenyewe mashabiki wataingia kama kawaida, lakini mechi ya Jumatatu ya Sampdoria bado hawajatoa uamuzi.
Serikali ya Italia imewazuia wakazi wa miji ya kaskazini kutembea baada ya watu 229 kupatikana na virusi hivyo huku watu saba wakiwa wamekufa.
Mechi ya Inter Milan ya Europa Ligi hatua 32 bora dhidi ya Ludogorets kesho Alhamisi itachezwa bila ya mashabiki kutokana na kuhofia kusambaa kwa ugonjwa huo.
Inter ni moja ya timu nne za Serie A ambazo wiki iliyopita walihairisha mechi zao kutokana na hofu ya ugonjwa huo.
Vinara wa ligi Juventus wapo mbele kwa pointi moja kwa Lazio inayoshika nafasi ya pili kabla ya mchezo wake wa Jumapili dhidi ya Inter inayoshika nafasi ya tatu.
Ratiba ya mechi za Serie A zitakazochezwa bila ya mashabiki: Juventus v Inter (Jumapili); Udinese v Fiorentina (Jumamosi); AC Milan v Genoa (Jumapili; Parma v Spal (Jumapili); Sassuolo v Brescia (Jumapili)
Mechi za Serie A zitakazoshuhudiwa na mashabiki: Lazio v Bologna (Jumamosi); Napoli v Torino (Jumamosi); Lecce v Atalanta (Jumapili); Cagliari v Roma (Jumapili)