MABOSI wa Kampuni ya GSM ni kama wameshtukia kitu vile kutoka kwa watani wao wa jadi, Simba, ni baada ya jana kufikia makubaliano mazuri na kiungo wao fundi Mghana Bernard Morrison ya kuongeza mkataba mwingine wa kuendelea kukipiga Jangwani.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu ziwepo tetesi za kiungo huyo kuwaniwa na Simba wanaomtumia mmoja wa mawakala ili kufanikisha usajili wa kwenda huko kwa ajili ya kumtumia kwenye michuano ya kimataifa.
Morrison ni kati ya wachezaji sita waliosajiliwa na Yanga katika usajili wa dirisha dogo akitokea Motema Pemba ya DR Congo aliyokuwa anaichezea akisaini mkataba wa miezi sita pekee.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa na kuthibitishwa na Morrison mwenyewe jana mchana alikutana na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said kwenye moja ya hoteli kubwa kwa ajili ya kuzungumza na kiungo huyo na hatimaye kukubali kusaini mkataba mpya wa kuitumikia Yanga kwa miaka miwili.
Awali, Morrison alisema kuwa wapo kwenye mazungumzo mazuri na viongozi hao baada ya kufikia muafaka mzuri wa kuongeza mkataba mwingine wa kuendelea kukipiga Jangwani.
Aliongeza kuwa katika kikao hicho cha mazungumzo, alihusishwa Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael ambaye alishirikishwa kutoa maoni yake kuhusu wamuongezee mkataba au la.
“Mkataba wangu ulikuwa na usiri mkubwa kati yangu na viongozi, kwa kifupi nilisaini mkataba wa miezi sita pekee ya kuichezea Yanga ambao unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
“Hivyo, katika kuliona hilo, viongozi wameonekana kuvutiwa na mimi ndani ya kipindi kifupi na kuniomba niongeze mkataba mwingine wa kuendelea kuichezea Yanga.
“Na kutokana na sapoti kubwa na mapenzi makubwa niliyoikuta Yanga kutoka kwa viongozi na mashabiki, nimeshawishika kuongeza mkataba mwingine ambao ndani ya saa chache nitakutaarifu, bado nipo kwenye kikao na viongozi,” alisema Morrison.
Baadaye gazeti hili lilipata uhakika kuwa ameongeza mwaka mmoja na nusu, hivyo kuwa na mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea Yanga. Mshahara wake ukiwa ni dola 2500 kwa mwezi (Sh milioni 5.7).
Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) mchezaji akibakiza miezi sita kwenye mkataba wake anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine na ikiwezekana kusaini mkataba wa awali, lengo ni kulinda kiwango cha mchezaji kukosa timu ya kuichezea.