Korosho chafu ni majanga, wakulima watakiwa wachague " kusuka au kunyoa




Na Ahmad Mmow, Mbinga.
Wakulima wenye korosho zisizo na ubora wa kiwango cha madaraja ya kwanza na pili waliopo katika wilaya za Tandahimba na Newala , mkoani Mtwara, ambao watataka kurejeshewa korosho zao waandike na kupeleka barua za kuomba kurudishiwa. Iwapo hawatakuwa tayari kuuza kwa bei zinazofikiwa na wafanyabiashara.

Wito huo ulitolewa wilayani Newala mwishoni mwa juma lililopita na meneja wa chama kikuu cha ushirika cha Tandahimba Newala Cooperative Union( TANECU), Mohammed Mwinguku alipozungumza na waandishi wa habari ambao walimuomba aeleze hatima ya wakulima ambao watataka warudishiwe korosho zao iwapo hawataridhishwa na bei za wanunuzi.

Mwinguku alisema wakulima ambao wanataka kurejeshewa korosho zao kutokana na kutoridhishwa na bei waandike barua na kupeleka TANECU waombe kurudishiwa. Lakini wajiandae kubeba gharama.

Mwinguku alizitaja baadhi ya gharama zitakazobebwa na wakulima hao kuwa ni usafirishaji( shilingi 52.50 kila gunia moja),  kulipia gunia( shilingi 1,400 ), mtunza ghala( shilingi 38.00) na nyingine watakazoambiwa, iwapo zitakuwapo na watatakiwa kulipa.

Mbali na hayo, meneja huyo alisema katika mnada wa mwisho kwa korosho hizo, tani 450 kati ya 1,300 zilinunuliwa. Ambapo kila kilo moja ilinunuliwa kwa shilingi 975.

" Lakini pia wakulima wameomba wasamehewe tozo mbalimbali kwenye korosho hizo ili wapate bei nzuri. Tozo hizo ni ushuru wà chama kikuu, kituo cha utafiti cha Naliendele na halmashauri," alisema Mwinguku.

Hata hivyo Mwinguku alibainisha kwamba wakulima wanaimani na serikali kwamba itawatafutia wanunuzi na watakaonunua kwa bei nzuri. Lakini pia wanakiomba chama hicho kiendelee kutafuta soko. Kwani licha ya kuridhia kuuza kwa bei ya shilingi 975, lakini mnunuzi alinunua korosho chache.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad