Mahakama yatengua kufukuzwa kazi Mwalimu Oluoch


Mahakama ya Rufani nchini Tanzania imetengua hukumu ya Mahakama Kuu iliyoridhia uamuzi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kumwondoa kazini Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekia Oluoch.

Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo waliosikiliza rufaa hiyo, lililoongozwa na Jaji Sivangilwa Mwangesi, akishirikiana na majaji Mwanaisha Kwariko na Rehema Kerefu.

Katibu Mkuu Utumishi aliamuru Oluoch ambaye alikuwa mwalimu wa shule ya sekondari Tambaza kuondolewa kwenye utumishi wa umma mwaka 2017 kwa madai ya kushindwa kutekeleza masharti ya kuamua ni nani wa kumtumikia kati ya mwajiri wake au CWT.

Oluoch alifungua shauri la maombi Mahakama Kuu Masjala Kuu akiiomba ifanye mapitio na kisha kutengua uamuzi wa katibu mkuu Utumishi.

Mahakama hiyo katika uamuzi uliotolewa na Jaji Pellagia Khaday, April 18, 2018, iliyotupilia mbali maombi yake ya kutengua uamuzi wa katibu mkuu utumishi wa kuamuru aondolewe katika utumishi, ikisema kuwa hayana mashiko, ndipo akakata rufaa hiyo akipinga hukumu ya Mahakama Kuu.

Katika rufaa hiyo, wajibu rufaa walikuwa ni Katibu Mkuu Utumishi, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Katibu Mkuu Ofisi ya Raisi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Katibu wa Tume ya Walimu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Mahakama ya Rufani katika hukumu hiyo imesema kuwa katibu mkuu utumishi hana mamlaka ya kumwondoa mtumishi wa umma katika utumishi.

Katika hitimisho lake baada ya kusikiliza na kujadili hoja za pande zote na kurejea sheria na kanuni za utumishi wa umma, kwa tafsiri isiyo rasmi mahakama hiyo katika hukumu hiyo ambayo Mwananchi imeiona nakala yake imesema;

“Kutokana na hoja hizo hapo juu ni mtizamo wetu kwamba katibu mkuu Utumishi alivuka mamlaka yake kwani hana mamlaka ya kutoa amri ya kumwondoa mtumishi wa umma katika utumishi.”

“Iko wazi kwamba kumuondoa au kuagiza kuondolewa kwa mwalimu katika utumishi si miongoni mwa mamlaka ya mrufani wa kwanza (Katibu Mkuu Utumishi) ya kisheria.

Hata hivyo mwalimu anaweza kuondolewa katika utumishi wa umma na Rais kama inavyoelezwa katika kanuni ya 29 (1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma.

SOMA HABARI HIZI KIRAHISI KUPITIA APP YETU YA UDAKU SPECIAL DOWNLOAD HAPA

Chanzo: Mwananchi

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad