Mahakama yatoa hati ya kukamatwa Jacob Zuma



Mahakama ya juu ya Pietermaritzburg nchini Afrika Kusini imetoa hati ya kukamatwa kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma baada ya kushindwa kufika mahakamani kukabiliana na mashtaka kuhusu rushwa dhidi yake.

Hati hiyo itafanya kazi ikiwa atashindwa kuhudhuria kesi yake itakayoanza mwezi Mei. Bwana Zuma anakabiliwa na makosa 16 ya kughushi, rushwa , ulaghai na utakatishaji fedha ukihusisha biashara ya silaha ya thamani ya mabilioni ya dola iliyofanywa tangu miaka ya 1990.

Rais huyo wa zamani amefanikiwa kukwepa shutuma za rushwa dhidi yake kwa zaidi ya miaka 10. Lakini leo, sheria haikuwa upande wake.

Hati ya kukamatwa kwake imetolewa baada ya kushindwa kufika mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi yake. Jopo la wanasheria wake waliwasilisha nyaraka wakisema kuwa mteja wao alikuwa mgonjwa na amekuwa akipatiwa matibabu nje ya Afrika Kusini tangu mwezi uliopita.

Jaji Dhaya Pillay alihoji maelezo yaliyo kwenye nyaraka za matibabu za Zuma zilizowasilishwa na mawakili wake mahakamani. Lakini rais huyo wa zamani atakamatwa ikiwa atashindwa kufika mahakamani tarehe 6 mwezi Mei kesi yake itakapoanza rasmi.

Bwana Zuma anakabiliwa na mashtaka kadha wa kadha ya rushwa ikihusisha malipo 783 yenye utata anayodaiwa kupokea kutoka kwa aliyekuwa mshauri wake wa masuala ya fedha Schabir Shaik.

Madai hayo pia yamerejelea mkataba wa silaha uliofanyika miaka ya 1990 na kampuni moja ya masuala ya ulinzi ya nchini Ufaransa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad