Mambo Matatu yametajwa na Chadema Mwambe Kurudi CCM



Mtwara. Mambo matatu yametajwa na wanachama wa Chadema baada ya mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe kurejea CCM ikiwa ni takribani miaka mitano tangu alipokihama chama hicho tawala.

Wakati baadhi wakisema walimtarajia kurudi CCM kwa kuwa lengo lake ni ubunge, wapo wanaosema ni haki yake ya kikatiba kuamua chama anachokitaka kwenda huku wengine wakisema amehama baada ya kukosa uongozi Chadema.

Akiwa Chadema, Mwambe aligombea uenyekiti Kanda ya Kusini na kushindwa. Pia aliangukia pua katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Taifa.

Katika uchaguzi huo, Mwambe alipata kura 59 sawa na asilimia 6.2 huku Freeman Mbowe akipata kura 886 (asilimia 93.5).

Mwambe alitangaza uamuzi wa kuhama Chadema jana akiwa na katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole na kutumia nafasi hiyo kueleza kasoro kadhaa ndani ya Chadema, ikiwamo kukosa uhuru wa kuhoji masuala mbalimbali.

Mwambe anakuwa mbunge wa nane wa Chadema kujiunga na CCM tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kuhusu hatua hiyo, naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema: “Bwana ametoa, bwana ametwaa jina lake litukuzwe.”

Lakini katibu wa Chadema Kanda ya Kusini, Philbert Ngatunga alisema kuhama ni hiari.

“Ni pigo kuondoka kwake kwa sababu alikuwa mwanachama wetu. Kimsingi athari zipo na kuhama ni hiari ya mwanachama,” alisema Ngatunga.

Mwanachama wa Chadema mkoani Mtwara, Happy Mfinanga alisema: “Amerudi CCM kwa sababu alikosa uenyekiti wa kanda na Taifa. Huenda hicho kimemuumiza, hata (Frederick) Sumaye naye aliposhindwa Pwani na kuamua kurudi CCM.”

Mwambe pia alikuwa na ombi kwa CCM.

“Kama mtanipokea leo na kunikaribisha, basi nipewe tena nafasi ya kugombea endapo mtaridhia na nitapata nafasi,” alisema Mwambe.

Alisema Chadema hakuna uwazi katika suala la mapato na matumizi na wanachama hawana nafasi ya kuhoji lakini wanaonufaika ni wachache.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad