Man City Waijia Juu Uefa Kisa Kufungiwa Miaka Miwili, Kukata Rufaa Cas



London, England. Manchester City wameikosoa UEFA baada ya kukumbwa na adhabu ya kufungiwa miaka miwili kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na wametbitisha kuwa watakatia rufaa uamuzi huo.

Klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England wamefungiwa kushiriki michuano ya Ulaya ya ngazi ya klabu  na kutozwa faini ya Euro 30 milioni (Sh. 75 bilioni) kwa kosa ‘siriasi’ la kukiuka kanuni za Uungwana wa Matumizi ya Fedha na kushindwa kuonyesha ushirikiano na shirikisho hilo la vyama vya soka vya Ulaya katika upelelezi wa jambo hilo.

City wamekutwa na hatia ya kuipotosha Uefa kwa kutumia vibaya mapato ya udhamini wao kati ya mwaka 2012na 2016. Man City wanaweza kukatia rufaa uamuzi huo katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (Cas), ambayo inaweza kuiahirisha ama kuitengua kabisa hukumu hiyo.


Uchunguzi dhidi ya klabu hiyo ulitokana na ripoti iliyochapwa na jarida la Ujerumani la Der Spiegel ikianika barua pepe na nyaraka zilizonaswa kutoka kwa wadukuzi maarufu, Football Leaks, ingawa City walipuuza tuhuma hizo wakisema zimetokana na “nyaraka zilizoibwa ".


Na City wamesisitiza kwamba “wanao ushahidi mzito" wa kusapoti kukanusha kwao kufanya kosa lolote na wamesema hukumu ilitolewa kabla hata ya uchunguzi haujafanywa.

"Manchester City imefadhaishwa na lakini haijashangazwa na tangazo hili la Uefa," taarifa ya klabu hiyo ilisomeka. "Klabu inadhamiria kutafuta haki kupitia chombo huru na inao ushahidi mzito wa kusapoti inachopigania.

“Desemba 2018, Bosi ya Uchunguzi wa Uefa alieleza hadharani uamuzi utakaotolewa na adhabu anayotaka wapewe Manchester City, kabla hata uchunguzi haujaanza.

"Kiufupi ni hivi, hii ni kesi ambayo imeanzishwa na Uefa, ikaendeshwa na Uefa na hukumu ikatolewa na Uefa. Kwa kuwa sasa kesi imemalizika na huku imetolewa, klabu itaenda kukata rufaa Cas haraka iwezekanavyo."

City wamepangwa dhidi ya Real Madrid katika hatua ya 16-Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku mechi yao ya mkondo wa kwanza ikipigwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid Februari 26.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad