Mangula Aonya Wagombea Wa CCM Uchaguzi Mkuu 2020....Watakaoanza Kampeni Mapema Watakatwa Majina Yao


Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Philip Mangula amewaonya wagombea wa viti vya udiwani na ubunge kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kuwa wale ambao wataanza kampeni mapema kabla ya muda muafaka pamoja na kutoa zawadi mbalimbali watakatwa majina yao.

Mangula amebainisha hayo  Februari 16,2020 kwenye ukumbi wa CCM mkoa wa Shinyanga wakati akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu, na kamati za siasa za Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga.

Amesema Chama Cha Mapinduzi CCM kina kanuni na taratibu zake hivyo wagombea wote wanapaswa kufuata kanuni na maadili ya chama.

Ametoa onyo kwa wagombea wote ambao wana nia ya kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kuwa wale ambao wataanza kampeni kabla ya muda hawatasita kukata majina yao.

“Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, tunataka taratibu, kanuni na ya chama zifuatwe kwenye kugombea nafasi za udiwani na ubunge, wale ambao wataanza kampeni kabla ya muda pamoja na kutoa zawadi tutafyeka majina yao, bali msubiri muda ukifika ndipo muanze kujinadi,” amesema Mangula.

“Tunataka nidhamu ndani ya chama, na hakuna jamii ambayo haina taratibu namna ya kuishi, hivyo kamati za siasa chungeni sana wagombea ambao wataanza kufanya kampeni kabla ya muda wachukulieni hatua, na mkishindwa sisi tutaiwajibisha kamati nzima,”ameongeza.

Pia amewataka wana CCM kuendelea kushikamana na kuwa wa umoja hasa kwenye kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, pamoja na kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura, ili chama kipate ushindi wa kishindo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, amemuhakikishia Mangula kuwa chama hicho kimejipanga vizuri kuelekea kwenye uchaguzi, ambapo hakuna hata kiti kimoja ambacho watakipoteza, kuanzia nafasi ya udiwani na ubunge, huku akiahidi kutekeleza maagizo ambayo ameyatoa ikiwamo wagombea kuanza kampeni kabla ya muda.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti maalumu mkoa wa Shinyanga Azza Hilal Hamad, amemuomba Mangula kupeleka salamu za pongezi kwa Rais John Magufuli, kutokana na kazi kubwa ambayo anaifanya, huku akibainisha namna alivyotekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ndani ya Miaka Mitano, kwa kufanya shughuli za kijamii kwa asilimia 80 ikiwamo sekta ya afya na elimu.

Pia amemuomba kwenda kulisemea tatizo la kutokamilishwa kwa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga, ambapo mwaka 2018 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipofanya ziara mkoani Shinyanya alitoa ahadi ya kukamilisha hospitali hiyo, ambapo mwaka 2019 ingeanza kutoa huduma lakini hadi leo hakuna kinachoendelea huku majengo yakikaliwa na popo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad