Marekani ina mpango wa kuwaondoa raia wake kutoka katika meli ya kitalii ya Diamond Princess, meli ilio na kiwango kikubwa cha mlipuko wa virusi vya corona nje ya China, maafisa wanasema, Meli hiyo imetengwa katika bandari moja nchini Japani tangu mwezi Februari .
Kati ya abiria 3,700 waliopo ndani ya meli hiyo, 218 wamepatikana na ugonjwa huo. Raia wa Marekani watapatiwa viti katika ndege ya serikali siku ya Jumapili, kulingana na ubalozi wa Marekani mjini Tokyo.
Takriban watu 1500 wamefariki kutokana na virusi hivyo duniani ambavyo chanzo chake ni mji wa Wuhan uliopo China.
Tume ya afya nchini China siku ya Jumamosi iliripoti vifo vipya 143, na kuongeza idadi ya waliofariki kufikia 1523. Wote isipokuwa wanne wa waathiriwa hao walitoka mkoa wa Hubei.
Watu wengine 2,641 wamethibitishwa upya kuambukizwa virusi hivyo na hivyobasi kufanya idadi ya walioambukizwa ugonjwa huo kufikia 66,492.
Nje ya China bara, kumekuwa na zaidi ya visa 500 katika mataifa 24 na vifo vitatu, vikitokea Hongkong , Ufilipino na Japani.
Mlipuko huo katika meli ya Diamond Princess unasemekana kutoka kwa mzee mwenye umri wa miaka 80 ambaye alishuka mjini Hong Kong kabla ya kupatikana na ugonjwa huo.
Abiria na wafanyakazi wanazuiliwa katika meli hiyo mjini Yokohama hadi siku ya Jumatano. Mamia ya raia wa Marekani ni miongoni mwa wale waliokwama na takirban 24 wamepatikana na ugonjwa huo.
Lakini katika barua yake, ubalozi wa Marekani mjini Tokyo umesema kwamba raia wa Marekani waliopo katika meli hiyo watapimwa kabla ya kuruhusiwa kupanda ndege itakayowarudisha nyumbani siku ya Jumapili.
Ndege hiyo inatarajiwa kusafiri katika kambi ya kijeshi ya Travis mjini California ambapo baadhi ya abiria watawekwa katika karantini kwa siku nyengine 14.
Mpango wa kuwatenga zaidi waliopo katika meli hiyo unaonekana kuwakera wengi.
Tungependelea kumaliza karantini iliowekwa katika meli kama ilivyopangwa, halafu kutusafirisha Marekani kwa mipango yetu, kuna ubaya gani na hatua hiyo? mmoja ya abiria hao Mathew Smith alituma ujumbe wa twitter.
Kambi ya kijeshi ya wanahewa wa Marekani ya Travis Airbase kwa sasa imewaweka karantini zaidi ya raia 200 wa Marekani waliotolewa mjini Wuhan.