Mwanamume mmoja ametimuliwa kwenye ndege ya Marekani kwa kuvalia mask ya gesi baada ya abiria wenzake kuingiwa na hofu, Vyombo vya habari vya Texas vinaripoti.
Mwanamume huyo alikuwa amevalia mask na kuabiri ndege ya shirika la ndege la Marekani iliyokuwa ikisafiri kutoka Houston kuenda Dallas siku ya Alhamisi.
Wahudumu wa ndege hiyo walimuomba atoe mask hiyo baada ya abiria wenzake kuanza kulalamika, lakini alikataa kufanya hivyo katika hatua ambayo ilisababisha ndege hiyo kucheleweshwa kwa karibu saa moja.
Mwanamume huyo alikatiwa tiketi ya kusafiri na ndege nyingine ambayo aliabiri bila hiyo mask.
"Nilimuona mtu akija kupanda ndege akiwa amevalia mask kamili ya gesi, hali ambayo kwa kweli si ya kawaida," abiria Joseph Say aliambia kituo cha Hauston ABC, KTRK.
"Mara baada ya hapo, watu waliokuwa kwenye viti vya nyuma walianza kuhoji hatua hiyo ,"alisema.
"Haungeliona uso wake. Haungeliweza kumtambua ni nani. Watu walikuwa na hofu huenda ameingiza kisiri kitu hatari ndani ya ndege na kuvalia mask hiyo kwa ajili ya usalama wake."
Bwana Say anasema mwanzano alidhania mask hiyo ni ya kujikinga dhidi ya virusi vipya vya corona, ambavyo vimeua watu 259 nchini China.
"Lakini niligundua uko tofauti na mask za kawaida, hali ambayo nilihisi sio ya kawaida," aliongeza.
"Tulichosikia kutoka kwa mwanamke aliyekuwa amekaa karibu naye alidai amesema anataka kuwasilisha ujumbe. Sijui ulikuwa ujumbe wa aina gani," Bw. Say alisema.