Marekani wasisitiza Tume Huru ya Uchaguzi, Serikali wajibu




UBALOZI wa Marekani nchini, umempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuahidi kuwa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu utakuwa huru na haki huku wakisisitiza kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Januari 21 Rais Magufuli katika hotuba yake kwenye hafla ya kukaribisha mwaka mpya aliyoiandaa kwa ajili ya mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa Ikulu jijini Dar es Salaam, aliwaeleza viongozi hao kuwa, wakati ukifika watakaribishwa kuja kushuhudia demokrasia Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo Rais Magufuli alisema “kama nilivyoeleza awali mwaka huu nchi yetu itafanya uhaguzi mkuu, zoezi la uchaguzi ni muhimu kwa nchi yoyote, inayofuata misingi ya kidemokrasia kama yetu.

“Kwa hiyo basi Serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utafanyika katika mazingira ya amani, uhuru na haki, na kama ilivyo kawaida yetu wakati ukifika tutazikaribisha nchi na taasisi mbalimbali kuja kuangalia uchaguzi wetu ili kujionea jinsi nchi yetu inavyokomaa katika nyanja ya demokrasia,” alisema Rais Magufuli.

Jana, Ubalozi wa Marekani nchini kwenye tovuti yake uliweka taarifa ya kumpongeza Rais Magufuli kwa ahadi yake hiyo huku ukipendekeza kuharakishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Ubalozi huo pia ulieleza matarajio yao ya kuwepo kwa uchaguzi wa amani ambao wagombea wote watakutana kwa amani wakieleza mawazo yao na kampeni zitakazofanyka katika misingi ya usawa.

“Tumetiwa moyo sana na hakikisho lililotolewa na Rais Magufuli hapo la Januari mwaka huu, kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 utakuwa huru wa haki na wenye uwazi pamoja na mwaliko wake kwa waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa.

“Tunatarajia uchaguzi ambao raia wote na wagombea wa vyama vyote wanaweza kukutana kwa amani, wakielezea mawazo yao na kampeni zitakazofanyika katika misingi ya usawa.  

“Tunatoa wito wa kuharakishwa kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura lenye uwazi, kuanzishwa kwa Tume Huru za Uchaguzi na kuteuliwa mapema kwa waangalizi wa uchaguzi wa kitaifa na kimataifa wa kuaminika watakaofuatilia uchaguzi kwa kipindi kirefu na kipindi kifupi,”ilisema taarifa hiyo ya Ubalozi wa Marekani.

Alipoulizwa na MTANZANIA Jumamosi kuhusu endapo muda uliobakia utatosha kwa ajili kuundwa Tume Huru ya Uchaguzi, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk. Wilson Mahera alisema bado hajaiona taarifa hiyo ya Ubalozi wa Marekani.

“Bado sijaiona ngoja kwanza noisome halafu tutalizungumzia na pia limekaa kikatiba zaidi hivyo ngoja kwanza tuione,”alisema Dk. Mahera.

Kauli ya Rais Magufuli juu ya uchaguzi huru na wa haki iliwaibua viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani pamoja na wanaharakati, wakihoji uwezekano wa uchaguzi kuwa huru na haki bila kuwepo tume huru ya uchaguzi.

Hata hivyo wengine walipongeza hatua hiyo na kuwa ni mwanzo mpya wa siasa nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dk Agustine Mahiga alisema hawezi kuzungumzia suala hilo hadi kwanza afanye mawasiliano na mamlaka husika.

“Hili si suala la uamuzi wa peke yangu, lazima kwanza nifanye consultation,” alisema Dk. Mahinga.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad