Simanzi imetawala katika kijiji cha Mjawa baada ya watu sita wa familia moja kuuawa kwa kuchomwa moto wakiwa wamelala, lakini kunusurika kwa mtoto mwenye umri wa chini ya mwaka mmoja kunabaki kuwa tukio la kushangaza.
Mtoto huyo wa miezi minne, Shaban Juma, ndiye pekee aliyenusurika katika tukio hilo lililotokea usiku.
Mtoto huyo alikutwa amelala nje ya nyumba hiyo ya udongo wakati watu wakiwasili katika nyumba hiyo ya Regina Kamali kujaribu kutoa msaada wakati nyumba hiyo ikiungua usiku wa Februari 8, 2020.
Taarifa za awali zinasema mwanamume ambaye alikuwa akiishi na Regina ambaye polisi imesema anaitwa Richard Yakub ndiye aliyechoma nyumba hiyo moto wakati mpenzi wake akiwa amelala ndani na ndugu wengine watano.
Polisi wamesema walikuta dumu la lita kumi lililokuwa na mabaki ya petroli likiwa nje ya nyumba hiyo.
“Tulipofika sisi tulikuta watu wengine ndio wakatuambia kuna mtoto ameokotwa nje ya nyumba, sasa nashindwa kuelewa ni huyo mhusika aliamua kumnusuru au watu wa ndani walimtupa,” alisema Agnes Kamali ambaye ni dada wa marehemu Regina.
Haikufahamika mtoto huyo ambaye ni mjukuu wa Agnes na ambaye pia ana majeraha madogo usoni, alitolewa nje na aliyewasha moto huo au alitupwa nje na watu waliokuwa ndani.
Alisema Januari 25, mwanamume huyo alihamisha vitu vyake na kuaga kuwa angerudi kwao Masasi kwa ajili ya kuanza maisha mapya.
“Tuliamini kabisa kuwa hayupo mji huu. Sasa siku hiyo usiku nimepigiwa simu kuwa nyumbani kwa mdogo wangu kunawaka moto. Nilishtuka kwa sababu najua idadi ya wanafamilia waliopo kule,” alisema.
“Tulitoka hapa kwa haraka na kufika kule alfajiri hatukufanikiwa kutoa chochote zaidi ya mjukuu wangu mmoja wa miezi minne ambaye hadi sasa sielewi aliponaje.”
Mshangao huo pia umeonyeshwa na kaimu kamanda wa polisi wa Rufiji, Richard Ngole.
“Hata sisi tumeshangaa,” alisema Kamanda Ngole.
“Tulifika, tukaambiwa kuhusu huyo mtoto. Imekuwa ngumu kuelewa alitolewa nje kabla ya tukio au alisahaulika nje wakati watu wengine wameingia ndani kulala.”
Kamanda huyo alisema tukio hilo limesababishwa na ugomvi wa kimapenzi na tayari mtuhumiwa Yakub anashikiliwa na jeshi hilo.
Aliwataja waliofariki kuwa ni Regina Kamali (39), Regina Ng’onda (19), Agnes Taimu (26) na mtoto wake anayeitwa Maimuna Jumaa mwenye umri wa miaka mitatu.
Mwingine ni Frida Mario (22) mkazi wa Jaribu Mpakani aliyekwenda kwa Regina, ambaye pia anajulikana kama Mama Ben, akiwa na mtoto wake Nuru Kipengele (4) kwa ajili ya kuomba kazi kwenye klabu ya pombe.
Kaimu kamanda huyo alisema kuwa polisi walipofika katika eneo la tukio walikuta ndoo ya lita 10 ikiwa na mabaki ya mafuta ya petroli ambayo yalitumika kuchoma nyumba hiyo.
Mwananchi ilifika kijijini hapo na kushuhudia mabaki ya vitu vilivyoungua ndani ya nyumba hiyo iliyokuwa ikitumiwa na mama huyo kuuza pombe za kienyeji.
Nyumba hiyo ambayo ipo katikati ya shamba la mananasi na miti ya matunda, kwa sasa inapakana na makaburi sita ya watu wa familia moja.
Agnes, ambaye pia amepoteza watoto wawili katika tukio hilo, alisema kuwa kwa muda mrefu kulikuwa na mgogoro kati ya marehemu na mtuhumiwa.
Kwa mujibu wa Agnes mgogoro huo ulishafika katika ngazi mbalimbali za usuluhishi-- kuanzia serikali ya kijiji, kata hadi polisi ambako uamuzi uliofikiwa ni wawili hao kuachana.
“Mama Ben na huyo mwanaume walikuwa na uhusiano wa miaka miwili. Walikutana tu huko barabarani wakapendana na kuanzisha mapenzi,” alisema.
“Marehemu ndiye alikuwa na mji. Huyo mtuhumiwa alikuwa anakuja na kuondoka. Yaani anaweza kuja akakaa siku tano akaondoka. Sasa inaonekana kulikuwa hakuna maelewano na mdogo wangu, akaamua kuumaliza uhusiano huo.”
Alisema baada ya mvutano, hatimaye viongozi wa kijiji na polisi wakaamua mtuhumiwa achukue kila kilicho chake na kuondoka katika nyumba ya marehemu.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Uponda Chini eneo ambako tukio hilo lilitokea, Sefu Sultan alisema siku hiyo alipokea simu saa 9:30 usiku na kupewa taarifa za moto.
“Nilifika eneo hilo nikiwa na majirani zangu wawili na kweli tulikuta moto umeshashika. Tulizima na kuingia ndani lakini hatukuweza kuokoa chochote,” alisema.
“Tulikuta watu wote waliokuwa ndani wameteketea, wanne wakiwa kwenye chumba kimoja. Inaonekana walikuwa wanajaribu kufungua mlango ambao ulikuwa umefungwa. Mmoja alikuwa kwenye korido mwingine chumba kingine.”
Alisema baada ya kukuta hali hiyo waliwataarifu polisi ambao walifika na kuanza shughuli zao za upelelezi.
Akizungumzia tukio hilo mkazi wa kijiji cha Uponda, Hamis Kiwope alisema limewaacha katika mshangao mkubwa kutokana na roho za watu wasio na hatia kuteketezwa.
“Nimezaliwa hapa. Nina miaka zaidi ya 80 sijawahi kukutana na kitu kama hiki. Imetushangaza na kutuhuzunisha mno kwamba tukio la kinyama namna hii limefanyika katika kijiji chetu,” alisema.