Mikel Obi abaguliwa Uturuki, Trabzonspor yalaani vikali
0
February 04, 2020
Uongozi wa klabu ya Trabzonspor inayoshiriki ligi kuu ya Uturuki, umelaani vitendo vya ubaguzi wa rangi alivyooneshwa kiungo kutoka nchini Nigeria John Mikel Obi, wakati wa mchezo dhidi ya Fenerbahce, uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32, alianza kukumbana na manno ya kibaguzi katika mitandao ya kijamii kutoka kwa mashabiki wa Fenerbahce kabla ya mchezo huo, na wakati wa mchezo hali iliendelea kuwa mbaya kwa obi Mikel.
Tayari uongozi wa Trabzonspor umethibitisha kufungua kesi ya kulalamikia hali hiyo, na unaamini watuhumiwa watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili kujibu mashataka.
FIFA kuimwagia fedha Afrika, yashauri mfumo wa AFCON ubadilishwe
“Ubaguzi wa rangi haukubaliki hata kidogo, kila siku umekua ukipigwa vita michezoni na kwenye sehemu nyingine katika jamii, hatutalifumbia macho hili ambalo daima linaonekana ni ujinga kwa watu wachache,” klabu ya Trabzonspor imeandika ujumbe huo kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Wachezaji wa Trabzonspor nao kwa pamoja wamelaani kitendo hicho, kwa kusema kimewachukiza, na wataendelea kuwa bega kwa bega na mwenzao John Mikel Obi.
Katika mchezo huo Trabzonspor ilifanikiwa kuibanjua Fenerbahce, mabao mawili kwa moja, na kuchupa kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ya Uturuki.
Mikel Obi alijiunga na klabu ya Trabzonspor mwaka jana (2019) akitokea Middlesbrough ya England, ambayo ilimsajili akitokea Tianjin TEDA Football Club ya China mwaka 2017.
Kiungo huyo ambaye aliwahi kuwa nahodha wa kikosi cha Nigeria, alipata umaarufu mkubwa duniani alipokua akiitumikia klabu ya Chelsea ya London (England) kuanzia mwaka 2006-2017.
Tags