Kiongozi wa Kanisa la Inuka Uangaze, Nabii na Mtume Boniface Mwamposa amesema kwa sasa amesitisha makongamano yote kutokana na tukio lililotokea hivi karibuni lililosababisha vifo vya watu 20.
Kiongozi huyo amesema hayo leo Jumapili Februari 09, 2020 katika viwanja vya Tanganyika Packers Kawe muda mfupi kabla ya kuanza ibada.
Watu 20 walifariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa Jumamosi Februari Mosi, 2020 mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro waliposhiriki ibada ya kiongozi huyo katika uwanja wa Majengo, wakigombea kukanyaga mafuta ya upako yaliyomwagwa milango ya kutokea uwanjani.
Kutokana na maafa hayo, Mwamposa amesema kusitisha makongamano kwa sasa na ratiba ya makongamano itatolewa baadaye.
“Kwa sasa makongamano mengi nimeyasimamisha kwa sababu ya jambo hili, tunaomba neema ya Mungu ikapate kusimama na watu na baada ya hapo ndipo nitaweka ratiba ya makongamano.”
“Kwa mfano leo (Jumapili) ilipaswa liwe kongamano kubwa la kukanyaga mafuta lakini kwa sababu ya shida iliyotokea, tumesimamisha yote kupata utulivu wa kuomba Mungu atupe neema ya kupanga mipango upya, nitaongea mengi kwenye ibada,” amesema Mwamposa.
Amesema kuwa tukio hilo kwake ni jaribu zito na ametoa pole kwa wote waliojeruhiwa na waliopoteza ndugu zao kwenye tukio hilo.
“Hili ni jaribu, natoa pole kwa watu wote ambao wamepatwa na hili tatizo wengine wameumizwa, wamefiwa ni jambo ambalo limetuumiza na kutusikitisha lakini namuomba Mungu awatie nguvu wote” amesema.
Amesema tukio hilo lilitokea wakati yeye akiwa tayari ameshaondoka Moshi kurudi Dar es Saalam ambapo alikuwa anawahi kongamano lingine.
“Unajua linapofika jambo kama hili kila mmoja atazungumza ya kwake, hatuwezi kuongea mengi kwa sababu tayari vyombo vya usalama vinachunguza jambo hilo,kwa hiyo nikiongea mengi nitavuruga uchunguzi wao.”
“Lakini ninachoweza kusema Jambo hili limetokea wakati mimi nimetoka nakimbilia Dar es Salaam kwenye kongamano.