JINA la Nandy linasikika zaidi barani Afrika kwenye anga la muziki wa Afro-Pop (Bongo Fleva ndani yake) kiasi cha kuwa mmoja wa wanamuziki wa kike nchini Tanzania ambao ngoma zao zinasikilizwa zaidi ndani na nje ya Bongo.
Jina lake kwenye Kitambulisho cha Taifa cha Nida ni Faustina Charles Mfinanga.
Mashabiki wengine wa Bongo Fleva wanamtambua kama The African Princess.
Ngoma iliyomtambulisha ilikuwa ni Nagusa Gusa ambayo Remix yake alifanya na Mr Blue au Byser Bablon Bizzy.
Kabla ya kufanya poa kunako Bongo Flevani, Nandy alikuwa mshindi wa kwanza katika Shindano la Karaoke Barani Afrika la Tecno Own The Stage lililofanyika Februari, 2016 kule nchini Nigeria.
Katika shindano hilo, Nandy aliibuka nafasi ya pili na kujizolea kitita cha shilingi milioni 36 za Kitanzania na kuahidiwa kuingia katika lebo kubwa nchini Nigeria ya Chocolate City na kufanya kazi huko.
Baadaye alijiunga na Jumba la Vipaji Tanzania (THT) na safari yake ya muziki ikakolea hadi sasa akiwa amekimbiza na anakimbiza na ngoma kibao kama Ninogeshe, Kivuruge, Aibu, Wasikudanganye, One Day, Hazipo na nyinginezo hasa zile za kushirikishwa kama Kiza Kinene na Bugana.
Nje ya muziki, Nandy ni bonge moja la dizaina kwa mastaa. Mavazi yake yote anayoonekana amevaa ya asili, huwa anabuni mwenyewe na kushona.
Miongoni mwa watu maarufu aliowahi kula shavu la kuwabunia mavazi kupitia kampuni yake ya The African Princess Print ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson.
Katika tukio la hivi karibuni la vifo vya watu 20 mjini Moshi waliokuwa kwenye Mahubiri ya Nabii na Mtume Boniface Mwamposa, Nandy ni miongoni mwa mastaa walioguswa zaidi! Unajua kwa nini?
Nandy anasema ni kwa sababu Mwamposa ni baba yake wa kiroho na amemsaidia vitu vingi. Kujua zaidi juu ya uhusiano wa Nandy na Mwamposa na mengine mengi, IJUMAA SHO-WBIZ inaku-letea maho-jiano maalum na mwana-dada huyo kwa mwaka 2020, ungana naye;
IJUMAA SHOWBIZ: Nandy hongera kwa kazi nzuri na ni muda sasa hatujafanya mahojiano tangu mwishoni mwa mwaka jana na sasa ni mwaka mwingine wa 2020…
Nandy: Asante… Mungu anatusaidia na kutuongoza kila siku, ninamshukuru mno kwa hilo.
IJUMAA SHOWBIZ: Mwaka huu kwako umeanzaje?
Nandy: Ni mwaka mzuri sana, umeanza kwa kismati kwa kweli. Nimepata ubalozi wa bidhaa kama tatu. Lakini niseme tu kwamba mwaka jana siwezi kuacha kushukuru kwani umeacha historia kwenye muziki wangu. Nilipata shoo nyingi sana. Nilifanya kazi kuliko mwaka mwingine wowote huko nyuma.
IJUMAA SHOWBIZ: Vipi kuhusu kuachia ngoma mpya mwaka huu?
Nandy: Hiyo haipiti hata wiki mbili nitakuwa nimetoa kitu kikali sana, mashabiki wangu wakae mkao wa kula na ninawaahidi pia kwamba mwaka huu Mungu akitujaalia uhai, basi itakuwa ni bandika-bandua.
IJUMAA SHOWBIZ: Kama ulivyosema, mwaka jana ulikuwa ni wa neema sana kwako, nakumbuka tulifanya mahojiano uliponunua gari la bei mbaya (Landrover Discovery 4) na uliniahidi kuwa muda si mrefu utahamia kwenye mjengo wako wa kifahari, vipi umeshahamia?
Nandy: Kiukweli ninamshukuru Mungu, mambo yameenda vizuri sana. Siwezi kuweka kila kitu wazi, lakini niishie tu kusema ninamshukuru Mungu, mengine ngoja ninyamaze watu wasije wakasema ninajiinua au kujimwambafai.
IJUMAA SHOWBIZ: Nakumbuka ulikuwa na ofisi na kampuni ya kudizaini mavazi, je, bado unaendelea?
Nandy: Bado ipo na inafanya vizuri tu na baada ya muda kuna kitu kingine ambacho ni mradi wangu mkubwa sana nitauweka wazi.
IJUMAA SHOWBIZ: Kutokana na mafanikio makubwa ambayo yanao-nekana kwenye muziki wako kiasi cha kuwafunika wengine ambao wameanza zamani, inadaiwa kuwa unatumia ndumba, je, ni kweli?
Nandy: Nikisikia hivyo huwa ninacheka sana kwa sababu situmii chochote ili niinuke kimuziki, badala yake ninafanya kazi kwa nguvu zote kila kukicha. Wanaosema hivyo wamuogope Mungu kabisa.
IJUMAA SHOWBIZ: Bado kuna stori nyingi mtaani na mitandaoni kwamba bado una bifu na mwanamuziki mwenzako Ruby. Je, uhusiano wako na Ruby ukoje?
Nandy: Mimi sina shida na mtu yeyote. Kama mtu ananichukia, ni yeye tu, lakini mimi sina tatizo kabisa.
IJUMAA SHOWBIZ: Naendelea kukupa pole juu ya kuondokewa na mchumba’ko, vipi kwa sasa upo kwenye uhusiano wa kimapenzi?
Nandy: Ndiyo ninaye. Tena nipo kwenye uhusiano ‘serious’ maana nisingeweza kukaa tu bila kuwa na mtu.
IJUMAA SHOWBIZ: Kuna mengi yanazungumzwa juu yako na msanii mwenzako, Billnas au Bilinenga. Je, nini kinaendelea?
Nandy: (kicheko) sitaki kuzungumzia hilo maana inawezekana pia huo uhusiano ‘serious’ niliouzu-ngumzia, inawezekana ndiye huyo, huwezijua.
IJUMAA SHOWBIZ: Nandy kwa sasa unaonekana kunenepa ghafla, kuna siri gani nyuma ya pazia?
Nandy: Labda ninakua au kingine inawezekana huo uhusiano ‘serious’ unanifanya niwe hivi. Lakini siri nyingine nakupa ni kwamba kwetu tuna miili mikubwa mikubwa.
IJUMAA SHOWBIZ: Najua una ukaribu na Nabii na Mtume Mwamposa. Je, unazungumziaje janga alilokutana nalo kule Moshi na matatizo aliyopata?
Nandy: Ni kweli mimi ninasali kwa Nabii na Mtume Mwamposa. Amekuwa baba yangu wa kiroho na amenisaidia vitu vingi sana.
Kuhusu tatizo alilopata, kwa kweli limeniumiza sana kwa sababu ninaelewa watu wanavyokuwa wanapoambiwa muda wa kukanyaga mafuta umefika. Huwa wanachanganyikiwa maana kila mtu anataka kukanyaga mafuta. Mimi ninamuombea sana janga hili lipite salama kwa kuwa naamini hakupenda litokee hivi lilivyotokea.