Nida yakwama Usajili wa Namba, vitambulisho



Dar es Salaam. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imeingia katika mkwamo kwenye hatua kadhaa za usajili wa namba za utambulisho wa Taifa (NIN) na vitambulisho hivyo, kutokana na hitilafu ya huduma za kimtandao.

Hali hiyo inayoathiri usajili wa laini unaoendelea kwa mfumo wa alama za vidole, ina maana kwamba watumishi wa Nida hawawezi kuingiza kwenye mfumo wa mtandao, taarifa za watu wanaohitaji namba na baadaye vitambulisho.

Mwananchi imedokezwa kuwa huduma za mtandao zilianza kuingia dosari Jumanne wiki iliyopita, zimekwamisha upatikanaji wa namba (NIN) kwa watu ambao laini zao za simu zimefungiwa kutokana na kutokusajiliwa.

“Mambo yamechacha Nida, wafanyakazi wanakwenda kukaa tu ofisini na hawafanyi lolote kwa sababu network provider (mtoa huduma za mtandao) alikuwa ameamua kukata huduma, huduma nyingi za Nida zimekwama kuendelea,” kilieleza chanzo hicho.

Juzi Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati wa Nida, Thomas Nyakabengwe alipoulizwa kuhusu changamoto hiyo alisita kutoa ufafanuzi akiomba kuwasiliana na idara ya masuala ya Tehama.

“Mpaka nipate consultation (mashauriano) na Mkurugenzi wa ICT kwa sababu mie siyo mtaalamu wa hiyo, unapozungumzia Network ni IT, kwa hiyo wacha nitafute majibu, nitakujibu,” alijibu Thomas huku akishindwa kuweka wazi iwapo kazi zimesimama au zinaendelea kwa sasa.

Jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene alikiri kuwapo kwa changamoto hizo za kimtandao tangu jioni ya Februari 13, mwaka huu, akisema tatizo si malipo kwa mkandarasi bali ni tatizo la kiufundi linaloendelea kufanyiwa kazi.

“Mtoa huduma za mtandao ni TTCL ambaye ni sehemu ya serikali, kwa hiyo haiwezi kuwa shida, na pesa si nyingi tushindwe kulipa,” alisema huku akikiri kwamba mkwamo huo umeathiri baadhi ya huduma zikiwamo za upatikanaji wa namba za utambulisho wa Taifa (NIN).

Simbachawene alisema taarifa za awali alizopata kutoka Nida, ni kweli kuna tatizo tangu Alhamisi na jitihada za kurejesha huduma hiyo zinaendelea kwa ushirikiano na wataalamu kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Kuna kifaa ambacho kiliungua, wanaendelea kushughulikia na maendeleo yanaweza kuwa mazuri leo (jana), mambo yakarejea kuwa sawa,” alisema Simbachawene akizitaja shughuli zilizoathirika kuwa ni pamoja na utoaji wa vitambulisho.

“Ili mtu asajiliwe kuna mambo mengi yanahitajika kutoka kwenye mikoa na wilaya zetu kwa hiyo mahusiano hayo yaliathiriwa na changamoto hiyo, lakini wakati wowote tukifanikiwa tutarejesha huduma,” alisema.

Meneja Uhusiano na habari wa TTCL, Puyo Nzayaimisi alikiri kwamba Nida ni wateja wao lakini akasema hana taarifa kuhusu changamoto za kimtandao.

“Ni kweli Nida ni wateja wetu wa huduma za kimtandao, wanalipia huduma hiyo kama wateja wengine, lakini sina taarifa zozote kuhusu changamoto waliyoipata,” alisema Nzayaimisi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyopo kwenye tovuti ya Nida, uchukuaji alama za kibaiolojia ni moja ya eneo linalotegemea hitaji la mtandao wakati wa hatua za usajili wa namba (NIN).

Hatua hiyo inajumuisha upitiaji wa taarifa za mwombaji katika mfumo, uchukuliaji wa alama za vidole, picha na utiaji wa saini ya kielektroniki huku mwombaji akitakiwa kufika katika ofisi za Nida au kituo cha usajili akiwa na nyaraka halisi kuthibitisha uraia na umri wake.

Hadi kufikia Januari 12, mwaka huu, laini milioni 10.3 zinazomilikiwa na watu milioni 3.2 zilikuwa kwenye hatua za uhakiki kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA).

Uzimaji na usajili

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano kwa umma wa TCRA, Frederick Ntobi aliahidi kufuatilia idara husika inayoweza kufanya uchambuzi wa athari zinazotokana na changamoto hiyo. “Ngoja nifuatilie idara inayohusika, nitakujulisha ila kwa sasa siwezo kujua athari.”

Kwa mujibu wa TCRA, hadi kufikia Februari 12, mwaka huu tayari jumla ya laini milioni 32.9 zilikuwa zimesajiliwa kwa mfumo wa alama ya vidole, sawa na asilimia 75.3 ya laini za simu milioni 43.7 zilizounganishwa mitandaoni.

Aidha, laini milioni 7.3 zilizimwa tangu Januari 20 hadi Februari 12 mwaka huu na tayari watumiaji wa laini milioni 1.7 wamerudisha laini zao kwa kusajili kwa alama za vidole hatua iliyopunguza idadi ya laini zilizozimwa kubakia milioni 5.5.

Alisema hadi sasa kuna idadi ya laini milioni 10.8 hazijasajiliwa zikiwa zinamilikiwa na taribani watu milioni 3.5. “Laini hizo zilisajiliwa kwa kutumia kitambulisho cha Mpiga kura na Mzanzibari Mkaazi. Uhakiki kwa kushirikiana na Nida unaendelea na utaratibu wa kuzifunga unatekelezwa.”

Kabla ya TCRA kuanza kuzima laini ambazo hazikuwa zimesajiliwa kwa mfumo huo, baadhi ya wananchi walionekana kulalamikia mara kadhaa kasi ndogo ya utoaji huduma za Nida lakini serikali ilitupia lawama wananchi kwa uzembe na tabia za kupuuza kampeni za usajili huo uliohitaji namba za Nida.

Tukio la usajili lilianza Mei mosi mwaka jana hadi ukomo wake Disemba 31 kabla ya kuongezwa siku 20 kulikofanywa na Rais John Magufuli.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad