Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amekataa kuidhinisha pendekezo la kuruhusu wanaume walio kwenye ndoa kufanya kazi kama makasisi katika jimbo la Amazon, uamuzi ambao ungetoa nafasi ya pekee kwa makasisi kutofuata kanuni ya useja ya kanisa hilo.
Wakati wa mkutano mkuu wa kanisa mwezi Oktoba, maaskofu wa jimbo la Amazon walipendekeza wanaume walio kwenye ndoa waruhusiwe kuwa makasisi ili kukabiliana na upungufu mkubwa wa watumishi kwenye jimbo hilo.
Katika tamko rasmi la kujibu mapendekezo hayo, Papa Francis hakuzungumzia kabisa suala hilo na pia amekataa pendekezo la kuruhusu watu wasio makasisi kutoa huduma ya sakramenti muhimu za komunio na kuungamisha waumini.
Kuondoa kanuni ya useja kwa makasisi wa jimbo la Amazon kungewakasirisha wahafidhina ndani ya Kanisa Katoliki ambao tayari wanauona uongozi wa Papa Francis unaochukua msimamo mkubwa wa kiliberali.