Polisi Tanzania Wamtaka Mwamposa Kujisalimisha


Jeshi la Polisi nchini Tanzania limemtaka mtume Boniface Mwamposa kujisalimisha mwenyewe polisi kwa mahojiano kutokana na vifo vya watu 20 vilivyotokea mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro jana usiku Jumamosi Februari Mosi, 2020.

Watu hao walifariki usiku wakati waliposhiriki kongamano la kidini uwanja wa Majengo, wakigombea kukanyaga mafuta ya upako yaliyomwagwa milango ya kutokea uwanjani.

Wakati Jeshi hilo likimsaka kwa udi na uvumba kiongozi huyo wa kiroho, Jeshi hilo linawashikilia watu saba akiwamo mchungaji wa Kanisa la Calvary Assemblies of God, Elia Mwambapa kwa mahojiano.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamduni akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Februari 2, 2020 amesema mchungaji huyo ndiye aliyeomba kibali cha kongamano hilo la siku tatu lililomalizika jana Jumamosi.

“Baada ya hilo tukio tumemtafuta sana huyo Boniface Mwamposa ambaye ni maarufu kwa jina la Bulldozer bila mafanikio. Kupitia kwenu tunamtaka ajisalimishe kwa mahojiano,” amesema

Kamanda Hamduni alifafanua kuwa idadi ya waliokufa ni 20 hadi sasa, ambapo kati yao watoto wadogo ni wanne, wawili wakiwa ni wa kike na watu wazima 16 wakiwamo wanawake 15.

Kwa mujibu wa Kamanda Hamduni, katika tukio hilo watu waliojeruhiwa ni 16 na wawili kati yao hali zao sio nzuri na kwamba kazi itakayoendelea kuanzia asubuhi ni kutambua miili ya marehemu iliyohifadhiwa Hospitali ya Mawenzi.

Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad