Polisi Yasema Aliyeuawa Singida Alikuwa dereva Bodaboda




JESHI la Polisi mkoani Singida limesema dereva wa bodaboda, Alex Jonas (40) aliyeuawa na watu wasiofahamika alikuwa siyo kiongozi wa Chadema. Jonas ambaye ni mkazi wa Majengo mjini Manyoni mkoani Singida mwili wake ulikutwa umepigwa na kitu chenye ncha kali Februari 25, 2020.

 

Kamanda wa Polisi, Sweetbert Njewike amesema dereva huyo ameuawa Februari 25 mwaka huu nyakati za usiku. Amesema kijana huyo ambaye kituo chake cha kazi kilikuwa Mwembeni mjini Manyoni bado haijafahamika siku ya tukio, aliondoka muda gani.

 

Kamanda Njewike amesema mwili wa marehemu uliokotwa mbungani mbali na barabara, ukiwa umechomwa chomwa sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kichwani na miguuni.

 

“Wakati mwili wa Alex ukiokotwa mbungani, pikipiki yake iliokotwa kandakando ya barabara iendayo Dodoma. Baada ya mwili kukaguliwa alikutwa na vitu vyote isipokuwa simu. Chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika, upelelezi unaendelea,” amesema.

 

Amesema hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na mauaji hayo ya kikatili na wameanzisha msako mkali.

 

“Tunaomba mwananchi yeyote mwenye taarifa sahihi juu ya tukio hilo atoe kwenye kituo chochote cha polisi kilicho karibu au mamlaka zingine ili watumtu aliyehusika aweze kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria,” amesema.

 

Kuhusu marehemu kuwa kiongozi wa Chadema wilayani Manyoni, Njewike amesema hilo wamelisikia lakini walipofanya utafiti imebainika kuwa alikuwa ni dereva wa bodaboda tu na sio kiongozi wa Chadema.

 

Wakati Kamanda Njewike akisema kuwa Alex hakuwa kiongozi wa Chadema, Mwenyekiti CCM Halmashauri ya Itigi, Alli Minja akizungumza na Mwananchi amesema marehemu Alex alikuwa mwenyekiti Chadema Wilaya ya Manyoni.

 

“Binafsi nasikitika kwamba sitohudhuria mazishi yake kutokana na kukosa usafiri. Alex alikuwa Chadema wa aina yake,” amesema na kuongeza;

 

“Alikuwa na utamaduni wa kuhudhuria vikao vya mabaraza ya madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na kwetu huku Itigi. Kwenye suala la miradi ya maendeleo, ulikuwa huwezi kujua kama ni wa upinzani. Alikuwa anatoa ushirikiano wa hali ya juu. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi,” amesema Minja.


Akizungumza leo na Mwananchi, mmoja wa viongozi wa Chadema Kanda ya Kati, Idd Kizota amesema wapo katika maandalizi ya mazishi ambayo yatafanyika wilayani humo Jumamosi, Machi 1, 2020.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad