Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amemuagiza Waziri wa TAMISEMI Seleman Jafo, kuhakikisha anamuandikia barua ya kumfukuza kazi mfanyakazi wa Wizara hiyo aliyechana na kuitemea mate Quran Takatifu mkoani Morogoro.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Februari 11, 2020, Jijini Dar es Salaam, wakati akiwahutubia wananchi wa Kigamboni muda mfupi tu mara baada ya kuzindua rasmi Wilaya hiyo na kusema kuwa Serikali haipo tayari kuwa na wafanyakazi wapumbavu.
“Juzi nilikuwa namsikia Mheshimiwa Jafo, mtu mmoja kule Kilosa nafikiri alichana kitabu kitakatifu, nashukuru umechukua hatua ya kumsimamisha kazi. Lakini mimi namfukuza moja kwa moja, muandikieni barua ya kuondoka moja kwa moja.
“Ashinde kesi, asishinde huyo siyo mfanyakazi wa Serikali. Hatuwezi tukakaa na wafanyakazi wapumbavu katika Serikali hii. Umechukua jukumu la kumsimamisha kazi lakini mimi namfukuza.
“Ninafahamu mlikuwa na matatizo na Ofisa Ardhi wa Kigamboni ni mtoro hajafanya kazi karibu miezi mitatu na alishaandikiwa barua kusudi ashughulikiwe lakini Wizara ya ardhi bado wanaleta mshahara wake ninajua hii meseji itafika kwao na huyo kama ni mtoro akatoroke moja kwa moja.
“Inawezekana mwaka huu ukawa mbaya kwasababu watu tumekalia kulalamika mafuriko na hatulimi baadaye maji yatakapopotea tutaanza kulalamika njaa na Mungu atatushangaa alituletea maji hatukuyatumia halafu atuletee jua ambalo halina mafuriko tuanze kulalamika njaa.
“Wakiwa na mafuriko huko, wewe unalima kunde. Wakiwa na mafuriko huko, wewe unafanya kazi ili baadaye watakapotoka wa kwenye mafuriko waje kula chakula chako kwa kuwatangwa pesa. Huo ndiyo ukweli ndugu zangu lazima niwaeleze,” amesema Rais Magufuli.