Rais Magufuli Ataja Sababu za Kumteua Dk Abbasi


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ametaja sababu ya kumteua Dk Hassan Abbasi kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo akisema ni kutokana na kufanya kazi nzuri ya kuisemea Serikali bila kuchoka.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Februari 3, 2020 katika hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua Ijumaa iliyopita.

Kabla ya uteuzi huo, Dk Abbasi alikuwa msemaji mkuu wa Serikali.

“Dk Abbas amefanya kazi nzuri kama msemaji wa Serikali, hakuchoka aliisemea vizuri Serikali, ningependa aendelee tu kuwa msemaji wa Serikali lakini mahali mtu anapotakiwa kupata promosheni, usimnyime promosheni.”

“Ndiyo maana tumemteua awe katibu mkuu wa wizara hiyo na kwa sasa hivi ataendelea kuwa msemaji wa Serikali mpaka tutakapopata mwingine na atakuwa anasema sasa akiwa mkubwa zaidi,” amesema Magufuli.

Viongozi walioapishwa leo ni pamoja na makatibu wakuu wapya Mary Makondo (Wizara ya Ardhi), Profesa Riziki Shemdoe (Viwanda na Biashara), Zena Ahmed Said (Nishati) na Christopher Kadio (Mambo ya Ndani).


Rais Magufuli amemuapisha naibu katibu mkuu wa Wizara ya Nishati, Leonard Masanja ambaye kabla ya kuteuliwa katika nafasi hiyo alikuwa kamishna wa umeme na nishati mbadala.

Wengine walioapishwa ni makatibu tawala wapya wa Mikoa mitatu, Judica Omari (Tanga), Stephen Mashauri (Ruvuma) na Emmanuel Turuba (Mwanza).

Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Brigedia Jenerali Suleiman Mzee aliyechukua nafasi ya aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Faustine Kasike ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.

Pia yupo naibu kamishna wa Magereza, John Masunga ambaye sasa ni kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, akichukua nafasi ya Thobias Andengenye ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Magufuli pia amemuapisha Nathaniel Nhonge kuwa kamishna wa Ardhi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Wilbert Chumakuwa ameapishwa kuwa msajili mkuu wa Mahakama huku Kelvin Mhina (msajili mahakama ya rufani) na Shamira Sarwat (msajili mahakama kuu).

Wengine walioapishwa ni Jaji Dk Gerald Ndika, Wakili Julius Bundala na wakili Genoveva Kato wanaokuwa makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad