NATUMAI hujasahau Marekani na Iran zilivyotunishiana misuli na vifua. Ni baada ya Marekani kumuua Mkuu wa Vikosi vya Misheni za Kimataifa na Oparesheni za Siri wa Jeshi la Iran (Quds), Jenerali Qasem Soleimani.
Si ndio Iran waliapa kulipa kisasi? Marekani wakasema "thubutuu!" Marekani waliahidi kuwashughulikia Iran endapo wangefanya shambulizi hata moja.
Kwani Waajemi huwa wanaogopa? Walipiga kweli. Rais Donald Trump akajifungia na majenerali wa Marekani, kujadili kuirudi Iran au kuipotezea.
Baada ya kikao kirefu, Trump na majenerali walitoa tamko la kutoingia vitani, sababu hakuna athari yoyote iliyotokea katika shambulizi la Iran.
Wakati huohuo, kukawa na maelezo ya Iran kwamba waliua askari wa Marekani zaidi ya 80.
Ukweli ni huu; hakuna askari yeyote wa Marekani aliyeuawa katika shambulio la Iran, lakini vifaa vya Marekani, viliharibiwa vibaya.
Kwa nini hakufa mtu? Jibu ni Saddam Hussein. Ni kwamba Marekani baada ya tishio la Iran, walijua Waajemi hawatanii, kwa hiyo wangekiwasha kweli.
Nini kilifanyika? Jibu ni Saddam Hussein. Askari wa Marekani, hawakulala kambini, walikwenda kujificha kwenye handaki lililojengwa na Saddam Hussein.
Ni handaki imara. Lenye uwezo wa kuhimili makombora mazito. Hivyo, wakati Waajemi wanashambulia, Wamarekani walikuwa kwenye maficho salama chini ya udhamini wa almarhum Saddam Hussein.
SOMA HABARI HIZI KIRAHISI KUPITIA APP YETU YA UDAKU SPECIAL
Ni kweli Wamarekani walijificha, hawakujeruhiwa na hawakuuawa, lakini ni salama asilimia 100? Aah wapi! Mpaka sasa imeripotiwa zaidi ya wanajeshi 100 wa Marekani wanaugua athari za ubongo kutokana na shambulizi la Waajemi.
Kwamba pamoja na kujificha kwenye handaki la Saddam, lenye uwezo wa kuhimili uzani wa makombora mazito, bado haikuwa salama salmini. Askari wa Marekani wanaugua athari za ubongo.
Ni jibu kuwa silaha za Iran zilizotumwa kambi za Marekani nchini Iraq zilikuwa nzito sana. Piga hesabu kama askari wa Marekani wasingejificha. Hali ingekuwaje?
Tatizo Wamarekani hata hawamshukuru Saddam. Japo walimpindua, wakasababisha anyongwe, lakini handaki lake ndilo lililowaokoa.
Ndimi Luqman MALOTO