Safari zote za Hija zapigwa Marufuku Kwa Muda Saudi Arabia


Serikali ya Saudi Arabia imezuia wageni wote wanaoingia nchini humo kwa safari za kidini, ikiwemo wanaotembelea miji mitakatifu katika dini ya Kiislamu - Makka na Madina.

Mamilioni ya watu huingia Saudia mwaka mzima kufanya ibada ya Umra, na wengi zaidi huingia kwa pamoja kufanya ibada ya Hija.

Tofauti na Hija, Umra hufanyika katika kipindi chochote cha mwaka, na kwa sasa marufuku hiyo inawalenga mahujaji raia wa nchi za nje wanaoenda kuitekeleza.

Bado haijulikani kama ibada ya Hija, ambayo inategemewa kuanza mwishoni mwa mwezi Julai kama itaathirika na zuio hilo pamoja na kusambaa kwa virusi vya corona duniani.

Saudia pia imewapiga marufuku watu kutoka nchi zilizokumbwa na virusi hivyo kuingia nchini humo.

Msikiti wa Madina ni wa pili kwa utukufu katika Uislamu na ndipo alipozikwa Mtume Muhammad.
Mpaka sasa Saudia bado haina mtu ambaye amethibitika kuambukizwa virusi hivyo.

Makka, ndio mji ambao Mtume Muhammad alipozaliwa, na kuna msikiti mtakatifu zaidi. Madina ndipo alipofariki na kuzikwa.

Wizara ya mambo ya nje ya Saudia inasema marufuku hiyo ni ya muda - lakini wizara hiyo haijataja lini marufuku hiyo itaondolewa.

Watalii ambao si wa kidini ambao wanatoka katika nchi ambazo virusi vya corona vimethibitisha kuingia pia watakataliwa kuingia Saudia.

Saudi Arabia imeeleza kuwa toka mwezi Oktoba imetoa viza zaidi ya 400,000 za watalii kutoka nchi mbali mbali duniani.

Shirika la Afya Duniani (WHO) mapema wiki hii limeonya kuwa dunia inapaswa kujiandaa kwa uwezekano wa janga la virusi vya corona.

WHO japo imesema kuwa ni mapema sana kuuita mlipuko wa virusi hivyo janga lakini nchi zinapaswa kuwa katika "awamu ya maandalizi".

Janga ni pale maambukizi ya ugonjwa yanaposambaa kwa urahisi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine katika maeneo mengi ya dunia.

Visa zaidi vya virusi ambavyo husababisha ugonjwa kupumua Covid-19, vinaendela kujitokeza, huku milipuko ya ugonjwa huo ikibainika katika mataifa mengi zaidi ya Uchina mabapo ndipo ulipoanzia.

Mpaka sasa zaidi ya watu 2,700 wameshafariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Toka virusi vya corona viripotiwe mwezi Disemba, zaidi ya watu 80,000 duniani, kutoka katika mataifa takribani 40 tayai wameshaambukizwa virusi hivyo. Wengi wao wakiwa nchini Uchina.

Iran (ambayo imetenganishwa na Saudia kwa mkondo mwembamba wa bahari) mpaka sasa imesharipoti vifo 19 - ambayo ni namba kubwa zaidi ya watu kwa mataifa ya nje ya Uchina.

Hata hivyo vifo hivyo vinatokana na wagonjwa 139, hali ambayo inawafanya madaktari wa magonjwa ya kuambukiza kuhofia kuwa nchi hiyo inaweza kuwa na wagonjwa wengi zaidi inaowaficha.

Barani Ulaya hali ni mbaya zaidi nchini Italia ambapo mpaka sasa watu 400 wamethibitika kuambukizwa ugonjwa huo kutoka watu 80 siku ya Jumanne. Watu 12 tayari wameshafariki nchini humo kutokana na mlipuko huo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad