Siku 150 nje ya Wasafi , Anguko lamtesa Harmo




DAR: Ikiwa ni takriban siku 150 tangu mwanamuziki anayefanya vizuri kunako gemu la muziki wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ aachane na Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), mkali huyo anadaiwa kuteswa na watu waliotabiri anguko lake, IJUMAA limesheheni.  Harmonize au Harmo aliachana rasmi na Lebo ya Wasafi mwishoni mwa mwezi Agosti, mwaka jana kisha kuanzisha lebo yake aliyoipa jina la Konde Music Worldwide (KMWW) ambapo alipoondoka kwenye lebo hiyo, mashabiki wengi, hususan wale wa mitandaoni waligeuka manabii na kutoa utabiri kuwa anguko lake limewadia.

Wengi walijenga hoja kwamba, hataweza kuhimili mikiki ya ushindani kwenye Bongo Fleva hasa kutoka kwenye lebo hiyo aliyoiacha iliyo chini ya mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

MCHAMBUZI AFUNGUKA

Mchambuzi wa masuala ya burudani, Erick Evarist ambaye pia ni Mhariri wa Magazeti ya Global Publishers, alipoulizwa kuhusiana na anguko hilo, alitoa mtazamo wake kwa kusema kitendo cha Harmo kuondoka Wasafi kilikuwa kipimo cha ukubwa wake.

“Huo ndiyo ulikuwa mtihani mkubwa kwa Harmo, kelele za anguko lake zilitawala sana na kila mtu alimfuatilia kwa karibu ili kuona kama kweli ataweza au atachemka,” alisema Evarist.

HARMO AWEKA BAYANA

Ili kujua hilo pamoja na mengine mengi kuhusu maisha ya nje ya Wasafi, Gazeti la IJUMAA lilimtafuta Harmo na kufanikiwa kuzungumza na meneja wake, Beauty Mmary ‘Mjerumani’ kwa niaba yake.

ASEMA WAPO VIZURI…

Mjerumani alianza kusema kuwa, kiujumla siku 150 za Harmo nje ya Wasafi ni za mafanikio makubwa na wanaelekea kuzuri zaidi. “Unajua Harmonize ni mwanamuziki ambaye siku zote amekuwa akifanya kazi katika malengo yake.

“Ana vitu ambavyo anaviweka na anatamani avifikie, tunapomzungumzia Harmonize yule ambaye alikuwa chini ya menejimenti f’lani (akimaanisha Wasafi) na huyu wa sasa ambaye ana lebo yake mwenyewe, ninaweza kusema hajabadilika kwa maana ya ku-drop (kushuka).

“Harmonize hajabadilika kwa maana ya kushuka kwa sababu ni tofauti na ilivyo kwa wasanii wengine ambao wakishatoka chini ya menejimenti f’lani na kuanza kujitegemea, basi utawaona wakipotea. Kwa Harmonize hilo ni tofauti kabisa na zaidi sana amepanda kiwango na anatamani afikie ndoto zake hasa kwenye anga za kimataifa,” alisema Mjerumani na kuendelea;

HODARI WA KUSHIRIKISHA UONGOZI

“Hali ni tofauti sana kwa msanii wangu, yeye ni yuleyule na tena anazidi kuwa bora zaidi na vitu vinavyomfanya asishuke ni kwamba huwa kila anachokifanya anashirikisha uongozi na sisi tunamshauri nini cha kufanya.

“Kama unavyoona sasa hivi amekuja na ajenda ya EP ya Afro-Beat (mjumuisho wa nyimbo chache) ambayo ameshirikiana na wasanii kibao kutoka nje wakiwemo wa Nigeria. “Hii ni kumfanya azidi kujulikana zaidi kimataifa.”

AZUNGUMZIA MALENGO

Meneja huyo alisisitiza kuhusu malengo yao kama uongozi; “Malengo yetu sisi kama uongozi ni kuhakikisha msanii wetu anakuja kuwa mwanamuziki mkubwa Afrika na duniani,” alisema Mjerumani.

VIPI KUHUSU SIASA?

Alipoulizwa kuhusu suala la msanii wake kudaiwa kuutema rasmi ule mchakato wa kugombea nafasi ya ubunge wa Jimbo la Tandahimba mwaka huu 2020, meneja huyo alisema kwamba kwa sasa wanahitaji msanii wao afike mbali zaidi kumuziki hivyo suala la siasa wameona ni bora waachane nalo kwa muda.

“Hili la Harmonize kuingia kwenye siasa kwa sasa mimi naona bado, sasa hivi tunataka ajikite zaidi kwenye muziki, halafu siasa itafuata baadaye,” alisema meneja huyo.

VIPI KUHUSU MGAHAWA? MBONA KIMYA?

Gazeti la IJUMAA lilimuuliza pia meneja huyo kuhusu ule mgahawa unaotembea aliouanzisha Harmo kwa lengo la kuwasaidia watu chakula cha bure, majibu yake yalikuwa haya;

“Mgahawa ni huduma ambayo ni endelevu na haijasimama. Kumepita ukimya kidogo kwa sababu tulikuwa bize ndiyo maana mnaona tupo kimya, lakini upo na hivi karibuni watu wataona tena tukigawa chakula kama tulivyofanya awali, lakini sasa hivi itakuja katika mfumo mwingine siyo ule uliozoeleka,” alimaliza meneja huyo.

HARMO NJE YA WASAFI

Tangu aondoke Wasafi, Harmo ameachia ngoma kadhaa ambazo zimedhihirisha kweli bado yupo sokoni kutokana na mapokeo.

Ameachia Uno, Kushoto Kulia na Hainishtui hivyo maneno ya meneja yanaakisi kazi ambazo zimezidi kumweka juu.

Kama hiyo haitoshi, Harmo amefanikiwa kulamba ubalozi wa juisi za Sayona, lakini pia kuandaa matamasha makubwa ya bure yanayodhaminiwa na kinywaji hicho.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad