WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amewataka watendaji akuu wa Jeshi la Polisi wawahoji watuhumiwa waliopo katika mahabusu ya vituo vya polisi nchini ili kujua makosa waliyoyafanya kama wanastahili kuwepo katika mahabusu hizo.
Simbachawene amesema lengo lake kuu la agizo hilo ni kudhibiti ubambikizwaji kesi ambao upo katika vituo mbalimbali nchini ambapo baadhi ya watuhumiwa wanapelekwa magerezani kwa makosa ambayo hawakuyafanya.
Akizungumza katika kikao chake na watendaji hao kilichofanyika ukumbi wa ofisi ndogo ya makao makuu ya jeshi hilo, jijini Dar es Salaam, jana, Waziri Simbachawene alisema maelekezo yake pamoja na ya Rais John Magufuli yanahusu masuala ya kesi na ubambikizaji wa kesi ambayo yapo katika baadhi ya vituo vya polisi nchini.
“Nawataka mfanye mchujo katika kesi za watuhumiwa mbalimbali waliopo mahabusu ambazo zinapelekwa mahakamani na watuhumiwa hao wanafanyiwa screening hata mara mbili au tatu kwa kuwahoji makosa yao uso kwa uso ili kuhakikisha mtuhumiwa huyo ndiye mwenye kesi ya mauaji, au ana kesi ya kubaka, au ana kesi ya wizi, na hata akipelekwa mahakamani awe ndiye anayestahili, ” alisema Simbachawene.
Pia aliwataka polisi kusimamia kwa hekima na busara suala la vijana wengi wanaoendesha bodaboda, kwa kuwa ni kundi kubwa na vijana ambao wamejiajiri kwa lengo la kupambana na ukosefu wa ajira nchini na duniani kwa ujumla.
“Isitafsiriwe kwamba ukiwaona vijana waendesha bodaboda ni watu wa hovyo hovyo; waendesha bodaboda wapo wenye digrii, diploma, kidato cha sita, wenye vyeti, wapo kidato cha nne. Si kundi la hovyo kama wanavyofikiri baadhi ya watu,” alisisitiza.
Aidha, Waziri Simbachawene aliwataka watendaji hao waendeleze ushirikiano walionao ili kuweza kupata njia ya mafanikio zaidi katika utendaji wa Jeshi hilo.
Kwa upande wake, Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro, alimshukuru Waziri huyo kwa kufanya kikao na viongozi wa jeshi lake, na alimuahidi kushirikiana na viongozi wenzake, ambapo watayafanyia kazi maagizo yote aliyoyatoa.
“Tumefurahi kumpokea mheshimiwa waziri hapa makao makuu madogo ya polisi, ni mara ya kwanza kufika hapa, na pia amezungumzia mambo mengi, yakiwemo maadili ya kazi, na pia amezungumza masuala ya uhalifu, amesema tupambane na uhalifu mapema kwa kuzuia kabla ya kutokea, na pia amezungumza masuala ya kushirikiana ndani ya Jeshi, na pia amezungumzia masuala ya bodaboda, na tunaahidi maagizo yote aliyoagiza tutayafanyia kazi,” alisema Sirro.
Waziri Simbachawene tangu ateuliwa na Rais Magufuli kuiongoza Wizara hiyo, baada ya aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, kangi Lugola, kuondolewa katika nafasi hiyo.