Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema, kama Bunge la Marekani linamshughulikia Rais wa nchi hiyo, Donald Trump kwa vitendo vya kukosa uzalendo, kwa nini isiwe hivyo kwa Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ambaye amefanya kitendo cha kuisaliti nchi Benki ya Dunia?
Spika Ndugai amesema hayo baada ya Mbunge wa Siha (CCM), Dkt. Godwin Mollel kuwasilisha hoja binafsi akiwashauri Wabunge wamuunge mkono kufikia uamuzi wa kumchukulia hatua Zitto kwa kitendo chake cha kuandika barua Benki ya Dunia (WB) akitaka Tanzania isipewe mkopo wa Dola milioni 500 kwa ajili ya Sekta ya Elimu
Spika Ndugai amewaambia Wabunge kuwa, Jimboni kwa Zitto kuna baadhi ya shule kuna wanafunzi hawana madawati wanakalia vigoda vya miguu 3 na kuna Shule ya Sekondari ina vyoo viwili, kimoja kinatumiwa na watoto wa kike na kingine kinatumiwa na wavulana
Spika Ndugai amesema, kitendo cha Zitto ni usaliti kwa kuwa fedha hizo zingesaidia kuondoa changamoto nyingi kwenye Sekta ya Elimu