Sumaye Ataja Sababu Kurejea CCM



Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani nchini Tanzania, Frederick Sumaye leo Jumatatu Februari 10, 2020 amerejea CCM, akibainisha kuwa amechukua uamuzi huo ili apate sehemu ya kutoa mawazo na ushauri wake.

Amerejea CCM takribani miezi miwili tangu alipotangaza kuwa si mwanachama wa Chadema.

Desemba 4, 2019 Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu mwaka 1995 hadi 2005 katika Serikali ya Awamu ya Tatu, alijivua uanachama wa Chadema na kumuachia ujumbe mwenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe.

Alijiondoa Chadema siku chache baada ya kupigiwa kura 48 za hapana kati ya 76 katika uchaguzi wa uenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani.

Sumaye alieleza kuwa kutokana na yaliyotokea kwenye uchaguzi huo na yeye kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti wa Chadema akipambana na Mbowe haoni haja ya kubaki katika chama hicho.

Lakini leo amerejea CCM, akitangaza uamuzi wake huo mbele ya katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally katika kikao cha baraza la wadhamini kilichoanza leo asubuhi. Dk Bashiru alikuwa  mgeni rasmi katika kikao hicho.

 “Nimekuwa waziri mkuu kwa miaka 10 na kiongozi kwa miaka kadhaa nitakuwa sitendi haki endapo nitakaa mahali bila kutoa ushauri au mchango wangu kwenye Taifa.”

 “Huwezi kutoa mchango kama hauna mahali na ukiutoa barabarani watu watakushambulia, nikaona mimi sio wa hadhi ya kufika kudharauliwa. Nikasema ngoja nirudi kwenye chama changu kilichonilea, kunikuza hadi nilipofika na kujivunia kuwa nina mchango katika Taifa hili,” amesema Sumaye huku akipigiwa makofi na wajumbe wa mkutano huo.

Huku mara kadhaa akisema CCM oyeee, Sumaye amesema amerudi CCM ili aendelea kusaidiana na wanachama wenzake na wananchi wengine kukijenga chama hicho tawala nchini Tanzania.

 “Bila kuwapotezea muda nimeamua kurudi kwa sababu hii, matumaini niliyoyategemea ya kusaidia nchi tu, shida yangu ilikuwa ni nchi tu. Mimi nina uzalendo ambao hauwezi kuutilia shaka na nilikuwa naangalia mbele sana kwa maslahi ya nchi, lakini imeshindikana.”

 “Nimekuja huku tujenge chama chetu na nchi, kama kuna dosari za hapa na pale nitakuwa na sehemu ya kusemea na nitawashauri viongozi akiwamo katibu mkuu. Nikiwa ndani ya chama nina nafasi kubwa ya kutoa mchango wangu, naomba mnipokee ndugu zangu,” amesema Sumaye.

Awali, Dk Bashiru amewaomba wanachama wa CCM kumpokea Sumaye, atakabidhiwa kadi yake katika makao makuu ya CCM Dodoma,  na muda ukiwadia atapokelewa kwa kishindo.

 “Nimefurahishwa sana kukupokea na heshima hii nitaiwasilisha mbele ya kikao cha kamati  kuu kitakachofanyika Jumatano ya wiki hii,” amesema Dk Bashiru.

Spika mstaafu wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho amesema wamekubali kumpokea Sumaye ili washirikiane kutoa mawazo yakihitajika.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad