Tetesi za usajili: Wanaotajwa Kuzihama Klabu zao Mwishoni mwa Msimu wa 2019/20
0
February 07, 2020
Kuna uwezekano wa Adama Traore akarejea katika ligi ya Hispania.
Manguli wa ligi ya nchini humo La Liga (FC Barcelona na Real Madrid) wametajwa kuwa kwenye mipango ya kuiwania saini ya nyota huyo wa klabu ya Wolverhampton Wanderers ya England.
Manguli hao wametajwa kwa nyakati tofauti na vyombo vya habari vya Hispania, kufuatia kuridhishwa na kiwango chake tangu alipotua England akitokea FC Barcelona mwaka 2015.
Traore alijiunga na Aston Villa mwaka 2015, mwaka mmoja baadae aliuzwa kwenye klabu ya Middlesbrough aliyoitumikia kwa miaka miwili (2016–2018), na kisha alisajiliwa na Wolverhampton Wanderers.
Gazeti la Gazzetta dello Sport ya nchini Italia limeripoti klabu ya Manchester United imeonyesha nia ya kutaka kumsajili nahodha na mshambuliaji wa FC Barcelona Lionel Messi.
Matumaini ya mshambuliaji huyo kuendelea kubaki Camp Nou yameanza kupungua kufuatia kukwaruzana na mkurugenzi wa michezo Eric Abidal.
Klabu nyingine zinazotajwa kumuwania mshambuliaji huyo hatari ni Manchester City, Paris Saint-Germain, Inter Milan na Juventus.
Manchester United imemuwashia taa ya kijano kiungo kutoka Ufaransa Paul Pogba, ili kutimiza ndoto za kumuondoa klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu.
Kwa mujibu wa gazeti la The Sun la England, Pogba anawaniwa na klabu za Real Madrid Juventus, na tayari Manchester United wametaja Pauni milioni 150 kama ada ya kiungo huyo.
Uongozi wa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus umekutana na mshambuliaji Paulo Dybala, kwa ajili ya kujadili suala la kusaini mkataba mpya.
Kwa mujibu wa tovuti ya Tuttosport, Juventus wamejipanga kumsainisha mkataba mpya mshambuliaji huyo kutoka nchini Argentina, ambao utafikia kikomo Juni 2025.
Mkataba wa sasa wa Dybala unatarajia kufikia kikomo Juni 2022.
Gazeti la L’Equipe ya Ufaransa limeripoti kuwa beki kutoka nchini Brazil Thiago Silva ameonyesha nia ya kuendelea kuitumikia klabu ya PSG, lakini uongozi wa klabu hiyo umedhamiria kumuuza mwishoni mwa msimu huu.
Hata hivyo bado haijafahamika ni wapi beki huyo mwenye umri wa miaka 35, atauzwa endapo dhamira ya uongozi wa PSG itatimizwa mwishoni mwa msimu huu.
Gazeti la The Telegraph la England limeripoti kuwa klabu ya Leicester City inaongoza katika mbio za kuhitaji huduma ya mshambuliaji wa pembeni wa mabingwa wa Ulaya Liverpool, Adam Lallana.
Mkataba wa Lallana utafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, huku uongozi wa Liverpool ukiwa kimya katika harakati za kumsainisha mkataba mpya.
Klabu nyingine zilizoonyesha nia ya kuingia kwenye kinyan’nganyiro cha saini ya mshambuliaji huyo ni Tottenham, Arsenal na West Ham.
Mshambuliaji kutoka Colombia na klabu ya Galatasaray ya Uturuki Radamel Falcao ameingia kwenye rada za klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabian.
Hata hivyo mshambuliaji huyo bado amesisitiza anahitaji kubaki mjini Istanbul, kwa ajili ya kuendeleza harakati za kutumikia soka la nchini Uturuki.
Tags