VIDEO: Membe Asema Urais Chanzo cha Kufukuzwa uanachama CCM


Dar es Salaam. Aliyekuwa kada wa CCM, Bernard Membe amesema amevuliwa uanachama kutokana na nia yake ya kutaka kupambana na mwenyekiti wao, John Magufuli kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Membe na makatibu wakuu wawili wastaafu-- Abdulrahman Kinana na Yusufu Makamba-- walifikishwa mbele ya kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu kujibu mashtaka ya kinidhamu.

Waliingia matatani baada ya sauti zao pamoja na za wanachama wengine watatu, kusambaa katika mitandao ya kijamii zikizungumzia kuporomoka kwa chama hicho na uenyekiti wa John Magufuli.

Makamba amesamehewa makosa yake, Kinana atakuwa chini ya matazamio kwa miezi 18, kipindi ambacho hataruhusiwa kugombea uongozi, wakati Membe amevuliwa uanachama na hivyo hataweza kutimiza ndoto yake ndani ya chama hicho.

Kwa mujibu wa katiba ya CCM, nafasi ya kugombea urais iko wazi kwa mwanachama yeyote, lakini utamaduni wa chama hicho ni kumpa Rais aliyepo madarakani kuwania muhula wa pili, lakini Membe alitaka kuachana na utamaduni huo.

Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema tangu mwaka 2014, Membe amekuwa akionyesha mwenendo ambao si mzuri licha ya kupewa adhabu ambazo zililenga kumsaidia ajirekebishe.

 .

“Tatizo ni urais. Wala wasipindishepindishe. Mara oh maadili, eti sijui fanya nini. Shida kubwa ni urais,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Mtama alipozungumza na Mwananchi jana muda mfupi baada ya tangazo la kumvua uanachama.

Membe, ambaye alizungumza akiwa Afrika Kusini ambako anamuuguza mwanaye, alisema alipanga kumkabili Rais Magufuli kuomba ridhaa ya wana CCM kugombea urais katika uchaguzi wa Oktoba, na kwamba hilo ndilo lililosababisha kufukuzwa kwake.
“Nilitamani niwepo leo ili niwajibu papo kwa papo, lakini ni bahati mbaya kwamba sipo. Nilitarajia kurejea leo lakini nimeshindwa. Ninatarajia kurejea mapema wiki ijayo, na nitazungumza kila kitu,” alisema.
Ni adhabu aliyoitarajia
 “Kwa sasa nitakwambia mambo mawili; kwanza sikushangazwa na uamuzi huu maana nilijua kabisakabisa kwamba nitafukuzwa.
“Hilo nililitarajia na hata nilipokwenda mbele ya kamati ya maadili niliwambia kwamba fanyeni kile mnachokusudia kufanya. Nilishajua mwezi mmoja kabla kwamba nitafukuzwa uanachama.”

Alisema kwa mujibu wa taarifa alizozipata, mpango wa awali ulikuwa ni kufukuzwa yeye na Kinana.

Alipoulizwa nani alikuwa nyuma ya mpango huo, alijibu kuwa ni “mwenyekiti na katibu wake,” lakini hakuwataja majina.

Membe alisema alipoitwa mbele ya kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu jijini Dodoma Februari 6, 2020 miongoni mwa maswali aliyoulizwa ni kama ana mpango wa kugombea urais. “Niliwajibu kwamba ndiyo nitagombea na nakwambia…ningegombea wala nilikuwa sitanii,” alisema.

Alipoulizwa iwapo bado ana mpango wa kugombea licha ya kufukuzwa uanachama, Membe alijibu: “Ndoto huwa haifi.

“Katika nchi hii niliyopo alikuwapo mzee mmoja anaitwa (rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson) Mandela. Alipokuwa anakwenda gerezani aliulizwa ikiwa bado anakusudia kuongoza nchi, naye alijibu ‘time will tell and the people will speak’ (ni suala la muda na watu watasema)”.
Membe alisema hofu ya wale waliopanga kumfukuza ni kwamba kugombea kwake kungekigawa chama.
“Niliwahoji wanaogopa nini wakati wana uwezo wa kukata jina langu? Niliwaambia waniache nigombee halafu huko mbele wakate jina langu maana si uwezo wanao bwana,” alisema.
“Mpango huu ulikuwa ni adhabu kwanza halafu process (mchakato) nyingine zinaendelea na mimi nilijua mwezi mmoja kabla”.

Alipoulizwa ni nani aliyempa taarifa kuhusu kuwapo kwa mpango huo alisema: “Sikiliza, mimi nina watu wangu serikalini, nina watu ndani ya chama na nina watu ndani ya usalama”.

HIZI HABARI KAMA HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL DOWNLOAD APP YA UDAKU SPECIAL BLOG <DOWNLOAD HAPA>

Alisema CCM hawakuwa na mbadala wa adhabu nyingine dhidi yake kwani wangemsimamisha kushiriki shughuli za kisiasa, wangekuwa wanaingilia uhuru wa mahakama.

Alisema hiyo inatokana na kuwa na kesi Mahakama Kuu dhidi ya Cyprian Musiba ambaye alitoa matamshi dhidi yake.

“Kwa hiyo kwa namna yoyote ile wangenipa adhabu ya kunizuia kushiriki siasa ingekuwa ni contempt of court (kuingilia uhuru wa mahakama).”

Alisema anamuonea huruma Kinana kwa kupewa adhabu ya karipio kwa kuwa hakuwa na kosa.

“Mimi kosa langu ni kuutaka urais, sasa mzee Kinana kafanya kosa gani? Kosa lake ni kuandika barua kulalamikia kuchafuliwa? Kwa kweli nimesikitika,” alisema.

Ikiwa kauli ya Membe ni sahihi, mwanasiasa huyo anaweka rekodi ya kuwa mwanachama wa kwanza kufukuzwa CCM kutokana sababu za kutaka kuwania urais kwa kupambana na mwenyekiti wake.

Lakini wapo wengine waliotimuliwa, kupewa karipio, onyo au kusimamishwa uanachama kwa sababu tofauti, akiwemo aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Sofia Simba ambaye baadaye alisamehewa, na aliyekuwa mwenyekiti wa mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu.

VIDEO:

Source:Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad