SERIKALI imesema, Kanisa la Inuka Uangaze la Mchungaji Boniface Mwamposa, lina jukumu la kugharamia msiba wa watu 20 waliofariki wakati wa kukanyaga mafuta ya upako.
Na kwamba, taratibu za awali zinafanywa na serikali lakini suala la majeneza, kusafirisha watu na ndugu zao waliofika kwenye kanisa hilo, zinatakiwa kubebwa na kanisa lenyewe.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 3 Februari 2020 na Anna Mghwira, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ambapo amesema, wamekuwa wakiwasiliana na kiongozi mkuu wa kanisa hilo aliyeko Kenya ili kubeba jukumu hilo.
“Kwa kweli wao ndio wanaotakiwa kugharamia majeneza, usafiri wa kuwapeleka marehemu kwao pamoja na ndugu zao waliokuja kuwachukua,” amesema Mghwira.
Kiongozi wa kanisa hilo aliyemtaja kwa jina moja la Maboya na kwamba, amekuwa akimtafuta tangu jana bila mafanikio, lakini sasa tayari amepata namba yake rasmi na amemtumia ujumbe.
Amesema, ibada ya kuaga maiti hao imeanza leo saa tano asubuhi huku taratubu za awali zikiendelea kufanyika.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Februari Mosi, 2020 baada ya kongamano la kidini ambapo waumini hao walikuwa wakigombea kukanyaga mafuta ya upako, yaliyomwagwa kwenye mageti ya uwanja wa Majengo.
Kibali cha kongamano hilo la siku tatu, kiliombwa na Elia Mwambapa, Mchungaji wa Kanisa la Calvary Assemblies of God na kwamba, mchungaji huyo aliomba mafuta hayo kutoka kwa Mchungaji Boniface Mwamposa.
Mpaka sasa Mchungaji Mwambapa na Mwamposa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na tukio hilo.