Wabunge CCM presha zaanza kupanda


Siku za hivi karibuni kumekuwapo na maonyo makali ya viongozi wa juu wa CCM dhidi ya makada wao wanaoonyesha nia ya kugombea ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Maonyo na makaripio haya hayana tafsiri nyingine zaidi ya kutoa taswira kuwa katika baadhi ya majimbo, kuna moto wa chinichini unawaka na kuwatia presha wabunge wanaomaliza muda wao. Hali hii imewafanya tangu kuanza kwa mwaka huu, baadhi ya wabunge wanapokuwa bungeni kuhudhuria vikao mbalimbali vya bunge, wanajikuta mwili uko bungeni lakini akili iko majimboni.

Hii inatokana na baadhi ya watia nia ndani ya CCM kukiuka maagizo ama kukaidi maelekezo ya kikanuni na miongozo juu ya kutofanya kampeni kabla ya kupulizwa kipenga na chama chao.

Hii imewafanya viongozi wakuu wa CCM, kila wanaposimama awe ni katibu mkuu, Dk Bashiru Ally au Makamu mwenyekiti, Philip Mangula au Makamu wa Rais Samia Suluhu wakemee hili.

Akiwa ziarani mkoani Tanga, Dk Bashiru alisema wako watia nia wameanza kutoa hongo ili kuandaa mazingira ya kuteuliwa kugombea uchaguzi mkuu 2020.

“Mnauza kura kwa miaka mitano kwa Sh 15,000 na Sh 20,000?” alihoji Dk Bashiru na kusema baadhi ya watia nia wanazunguka usiku kwenye baa, wakigawa fedha na vitu ili ‘kushawishi’ uamuzi.


“Wanazunguka na sukari, vitenge na Sh5,000 na Sh10,000. Hiyo ni dharau na ni matusi kwa mpiga kura. Waache. Tusiache misingi ya haki katika kutafuta wagombea,” alinukuliwa Dk Bashiru.

Alikemea pia baadhi ya watia nia wanaopita wakijinadi kuwa wao ndio wanaotakiwa na Rais John Magufuli na kuviagiza vikao vya uamuzi kuhakikisha hawapitishi watu wa aina hiyo.

Katika mkutano wake na viongozi wa CCM Februari 14, 2020, wilayani Sengerema, Mangula alionya makada wanao pitapita mitaani kusaka ubunge na udiwani kuwa watakatwa majina mchana kweupe.

Lakini Samia akitembea katika muktadha huo huo, akiwa katika maadhimisho ya miaka 43 ya CCM Mkoani Dar es Salaam, aliwaonya walioanza kusaka nafasi hizo wakati muda rasmi bado.

Kauli za wakubwa hao watatu zina tafsiri moja tu kuwa ubunge na udiwani safari hii ni pasua kichwa kwa baadhi ya maeneo, huku baadhi ya viongozi wakitajwa kuwa na wagombea mifukoni.

Katika baadhi ya majimbo ambayo pengine Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM anatajwa kugombea, kumekuwa na mitafaruku, Mbunge anaona pale M-NEC anapofanya ziara za kichama pengine anajijenga kisiasa.

Hali ya mtifuano haiko tu kwa wabunge wa majimbo, la hasha, bali hata kwa watia nia wa viti maalumu ndani ya CCM nako ni sokomoko kila mmoja akijaribu kumchongea mwenzake kwenye chama.

Pengine vita hii ivifanye vyombo vyetu kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Idara ya Usalama wa Taifa kuingia kazini kusudi vizuie Taifa kupata viongozi wasio na sifa.

Wabunge, Makada wafunguka

Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga alisema kinachofanywa na baadhi ya watia nia si sawa kwa kuwa Bunge halijavunjwa na linatarajiwa kuvunjwa na Rais Magufuli Julai 30, mwaka huu.

“Kwa hili karipio la Katibu mkuu na wengine nawapongeza sana. Kukiwa na watu ambao wanapita majimboni wanadhoofisha utendaji wa wabunge waliopo majimboni,” alisema Mlinga.

“Tukiruhusu hili, maana yake wabunge mwaka huu wote hawatafanya kazi za kibunge watakuwa wanalinda majimbo. Tunashukuru amelikemea hili kwa mustakabali wa chama na nchi,” alisema.

Mjumbe wa NEC, Joseph Tadayo alitumia maneno ya Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari ambaye alisema kama wasipoiua rushwa, basi rushwa itaiua Nigeria.

Tadayo alisema karipio la Dk Bashiru lisiishie tu kwa watia nia, bali hata wabunge waliopo madarakani ambao nao wanaweza kutumia zuio hilo kufanya kampeni kwa mwamvuli wa ubunge.

“Tuhakikishe harufu ya rushwa haisikiki kabisa kwenye chaguzi zetu za ndani. Hili haliendi tu kwa watia nia wapya, hata hao waliopo madarakani sasa,” alisisitiza na kuongeza;-

“Wapko wengi hawafanyi kazi zile za kibunge, wanasubiri dakika za mwisho zikifika waanze kufanya mambo yale ya juu juu tu lakini yanayowapa uhalali wa kutoa hongo.

“Wanatoa hongo ili warudi madarakani. Huo si ubunge wa CCM. Mtu anatakiwa kurudi hata kukaa milelele kwa sifa ya kutekeleza Ilani ya CCM na kuwahudumia wananchi,” anasema Tadayo.

Kada wa CCM aliyewahi kuwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli amempongeza Dk Bashiru, Mangula na Samia lakini akawaomba pia viongozi wa CCM wenye majina ya wagombea mifukoni.

“Baadhi wameanza kwenda vijijini na kwenye vikao wakisema huyu anapendwa na JPM (Rais) na huyu ndiye anayefaa achaneni na wengine. Hii ni hatari kwa sababu inawagawa wana CCM na inawagawa pia wananchi.

Mimi kwa maoni yangu, kiongozi ndani ya chama yeye ni baba wa watoto wote na baadhi ya viongozi wameona mbali na kwa mikoa kama Shinyanga, haya ndiyo yaliharibu mkoa siku za nyuma. Mwenyekiti Magufuli hana mtu. Sasa kama watu wa chini wanaanza kumsemea ni hatari.”

Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia alisema viongozi wameshaonya ni wajibu wa kila anayetaka kugombea kufuata maelekezo na kuheshimu kanuni za CCM zinazosimamia uchaguzi.

Ukisikiliza kauli za wabunge na historia ya migogoro iliyoinyima kura CCM katika baadhi ya majimbo, ni migawanyiko inayotokana na minyukano ya makada wakati wa kusaka ubunge na udiwani.

Hili pengine ndilo limeiamsha CCM mapema na haitaki kurudia tena makosa ya chaguzi zilizopita, na kuna dalili katika majimbo yenye msuguano, huenda jina likatoka kamati kuu.

Ndio, hili limefanyika katika chaguzi ndogo za majimbo ya Siha na Kinondoni ambapo wagombea walioteuliwa na CCM hawakupitia mchakato ule uliozoeleka wa kuchuana katika kura za maoni.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Sasa kichekeaho kiko Ilinga mchungaji kusikia STAA yuko njiani.

    Usiku Dozi ya PLESHA Asubuhi Dozi ya Sukali.

    Na Steve a a endelea na Mikwala yake ya Usanii. Mchungaji Hoi.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad