Wachina Wanne Waliomchapa Mkenya Kurudishwa kwao
0
February 13, 2020
Raia wanne wa Uchina waliokamatwa na Mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) wanatarajiwa kurudishwa kwao baada ya amri iliyotolewa na Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Fred Matiang'i.
Agizo hilo lilisainiwa na Matiang'i Jumatano baada ya mahakama kuruhusu polisi kuwashikilia wachina wanne kwa siku 15 huku uchunguzi ukiendelea juu ya tukio la kumchapa viboko raia wa Kenya aliyekua akifanya kazi katika mgahawa ulioendeshwa na Wachina hao mjini Nairobi.
Raia hao wa Uchina waliotambuliwa kwa majina; Ou Qiang, Deng Hailan, Chang Yueping, na Yu-Ling; walitiwa nguvuni Jumapili baada ya video iliyoonyesha mmoja wa wahudumu wa mgahawa wa wachina akipigwa viboko na mmoja wao katika mgahawa wao kueneo kwenye mitandao ya kijamii.
Katika video hiyo mwanaume wa Kichina alionekana akimpiga viboko Mkenya aliyekua akifanya kazi katika mgahawa unaouza vyakula vya kichina Chez Wou Restaurant katika eneo la Kileleshwa jijini Nairobi.
Iliripotiwa kuwa Mkenya, Simon Oseko, alikua akichapwa viboko kwa kosa la kuchelewa kufika kazini.
Alipigwa viboko viwili na meneja huku wafanyakazi wenzake wakishuhudia kwa mbali.
Oseko aliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi. Iliripotiwa kuwa mpishi wa Kichina katika mgahawa huo pia aliwatisha wafanyakazi wengine raia wa Kenya ili wasizungumzie kuhusu mateso wanayopitia katika mgahawa.
Walikamatwa kwa kumiliki vibali vilivyopitwa na wakati vya kuishi nchini Kenya na kufanya kazi nchini humo bila kuwa na vibali vya kazi. Baadhi walikua na vibali vya kutembea Kenya.
Balozi wa Uchina nchini Kenya Wu Peng amesema anaafiki hatua iliyochukuliwa na serikali ya Kenya dhidi ya Wachina hao wanne: ''Serikali ya Uchina na ubalozi wangu unawashauri Wachina binafsi na kampuni zinazowekeza nchini Kenya kufanya kazi kwa faida ya nchi iliyowapokea, na bila shaka kila mara tunawaomba raia wetu hapa kuheshimu sheria za Kenya na kuishi kwa amani na Wakenya, yeyote atakayevunja sheria atapata athari zake, uhusiano wa nchi zetu unategemea sio tu serikali zetu bali watu wa nchi zetu'' alisisitiza balozi Peng mjini Nairobi.
Raia wa Kenya walionesha hasira zao kwenye mitandao ya kijamii na wanaharakati na kudai hatua ya kisheria ichukuliwe kuhusiana na kisa hicho.
Jumapili, polisi walivamia mgahawa wa hoteli hiyo na kuwakamata wafanyakazi wanane raia wa kenya na raia wanne wa China kwa mahojiano.
Mwezi Juni mwaka jana Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang'i aliwatimua nchini humo wafanyabiashara saba wa kichina waliopatikana na hatia ya kufanya biashara zao kinyume cha sheria katika soko la maarufu la mitumba -Gikomba.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Wakenya wanaouza bidhaa zao kwenye soko hilo lililopo jijini Nairobi kulalamikia ongezeko la Wafanyabiashara wa Kichina ambao walidai kuwa wanawaajiri wenzao na kuleta ushindani wa biashara.
Wafanyabiashara katika soko maarufu la mitumba la Gikomba wanalalamika kuwa wachina wanawaajiri wachina wenzao kufanya kazi kama vile kupokea pesa na kuweka rekodi za mauzo, kazi ambazo hata wakenya wanaweza kuzifanya, huku wakiwakodisha wakenya kubeba mizigo kwa mikokoteni.
Tags