Wadau wa madini ya Tanzanite wa Mji Mdogo wa Mirerani, Simanjiro mkoani Manyara, wametakiwa kuchangamkia fursa ya madini hayo kwa kuwa serikali imeondoa kodi zilizokuwa zikilalamikiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula, aliyasema hayo jana wakati akizindua soko na mnada wa madini ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite.
Chaula alisema baada ya wadau wa madini kulalamikia kodi ya asilimia tano ya zuio na asilimia 18 ya ongezeko la thamani, aliwataka wadau kuchangamkie fursa hiyo.
Alisema serikali ina mpango na sekta ya madini ili iwe miungoni mwa sekta zinazochangia kwa wingi pato la taifa.
"Changamkieni fursa hizi za uuzaji na ununuaji wa madini kwa kuwa na soko hapa Mirerani na Orkesumet na soko lingine litafunguliwa hivi karibuni," alisema Chaula.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (Tamida), Sam Mollel, alishauri tozo hizo kutolewa kuwa kuwa zilikuwa tatizo kubwa kwa wadau wa madini.
Mollel alisema hali hiyo imehamasisha wachimbaji wadogo kuuza madini kwenye masoko ya madini kwa kuwa wana imani kodi zilizoleta usumbufu kwa wadau wa madini zimeondolewa na Rais Jophn Magufuli.
Katibu wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (Marema), Tariq Kibwe, alisema wadau wa madini wanaendelea kupewa elimu ya ulipaji kodi.
Mdau wa Madini ya Tanzanite, Shifonya Solomon alisema ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite, umekuwa na manufaa kwao.
Dalali wa Madini, Elisha Laizer alisema uwepo wa masoko ya madini ya vito ni nafuu kwao, kwa kuwa watapambana na matatizo mbalimbali yanayowakabili ikiwamo bei ya madini ya Tanzanite.
Salome Mnyawi, muuzaji wa magonga ya Tanzanite alisema, baadhi ya wanawake wa eneo hilo, watachangamkia soko hilo kupitia umoja wao.