Katika kuongeza Vivutio ndani ya Hifadhi mpya ya Burigi Chato, Simba wapato 17 maarufu kama Wafalme wa Pori, wamewasilishwa rasmi Hifadhini humo, kutokea Hifadhi ya Taifa Serengeti, tayari kwa kupandikizwa ili kuongeza chachu ya Sekta ya Utalii hapa Nchini, huku Simba hao wakipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brig. Jen. Marco E. Gaguti aliyemwakilisha pia Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Pichani Ni Miongoni mwa Magari ya Msafara yaliowabeba wanyama aina ya Simba wapatao 17, yakiwasili katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi - Chato kutokea Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Awali Dkt. Denis Kamba Mtafiti kutokea Taasisi ya Wanyamapori TAWIRI, ambae pia aliongoza msafara huo, akitoa maelezo kabla ya kukabidhi wanyama hao ameeleza kuwa, kwa sasa Tanzania ni Nchi pekee ambayo Inachangia nusu ya Simba wote Duniani, ikiwa na takribani Simba wapatao Elfu Kumi na Tano, huku akieleza sifa tele za aina ya Simba hao kutokea Serengeti ni tofauti na Simba wengine, na akiongeza Simba walioletwa Hifadhini humo wote ni familia moja na kati yao wamo madume wawili waliopewa majina ya Burigi na Chato.
Akieleza furaha yake kutokana na ujio wa Simba hao, Mkuu wa Mkoa Kagera Brig. Jen. Marco E. Gaguti hakusita kuzitaja faida za uwepo wa wanyama hao kuwa ni pamoja na kuendeleza kukuza uchumi wa Mikoa na Taifa, kupunguza matendo ya kiharifu na ujangili, mambo ambayo awali yalifanyika kwenye mipaka ya Hifadhi hiyo, lakini kubwa ikiwa ni kurejeshwa kwa moja kati vivutio ambavyo hupendelewa sana na watalii, huku akizidi kutoa shukrani zake kwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa maamuzi ya kuitangaza Burigi - Chato kuwa Hifadhi ya Taifa.
Naye Kamishina Mwandamizi wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi Martin Loibook amesema kurejeshwa kwa wanyama hao ambao walitoweka kufuatia sababu mbalimbali zikiwemo za kibinadamu kama vile ufugaji, zilizopelekea Simba hao kuuwawa kwa kuwindwa na wengine kutoweka, hivyo kurudishwa kwa Kundi hilo la wanyama wala nyama kutaongeza chachu ya watalii kufika Hifadhini Burigi - Chato kujionea Simba hao pamoja na Chui, ambapo pamoja na mambo mengine vivutio hivyo vitachochea pato la Taifa kwa watalii ambao watafika Hifadhini hapo.