Wakili Ataja Makosa ya Mwamposa na Wenzake
0
February 04, 2020
Moshi. Wakili mmoja nchini ametaja makosa yanayoweza kumkabili Mtume na Nabii, Boniface Mwamposa ambaye Jumamosi iliyopita aliongoza kongamano lililosababisha vifo vya watu 20 na 16 kujeruhiwa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Jeshi la Polisi lilitangaza kumkamata Mwamposa akiwa jijini Dar es Salaam na kusema litamrejesha mjini Moshi ili aweze kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo, sambamba na washirika wake wengine saba.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Salum Hamduni alisema kwa sasa hawezi kusema Mwamposa na wenzake wametenda kosa gani hadi uchunguzi utakapokamilika.
Hata hivyo, kumekuwa na hoja zinazokinzana katika mitandao ya kijamii, huko baadhi ya wachangiaji wakipendekeza ashitakiwe kwa uzembe uliosababisha vifo lakini wengine wakidai hana kosa.
Wale wanaotaka Mwamposa na washirika wake wasishitakiwe wanadai suala hilo ni la kiimani na Ibara ya 19 ya Katiba imetoa uhuru wa kuabudu.
Ibara ndogo ya kwanza inasema “Kila mtu anastahili kuwa na uhuru na mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake.
Lakini ibara 19 (2) inasema kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiyari la mtu binafsi na uendeshaji wake utakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.
Hata hivyo mmoja wa mawakili waliohojiwa na gazeti hili jana, alichambua msingi wa sheria na kutaja matendo ambayo kama yatathibitika, yanaweza kumfanya Mwamposa na wenzake kushitakiwa.
Wakili Julius Semali alisema Mwamposa na wenzake wanaweza kushtakiwa kwa mauaji ya bila kukusudia chini ya kifungu cha 195 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama kilivyorekebishwa 2002.
Tags