Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema wanaotaka kuongezwa kwa muda wa Rais kukaa madarakani kinyume cha katiba wana maslahi yao binafsi.
Akihojiwa na kituo cha ITV katika kipindi cha Kunani kuhusiana na maoni ya baadhi ya viongozi kutaka Rais kuongezewa muda wa kukaa madarakani kinyume cha matakwa ya katiba iliyopo sasa.
Jaji Warioba alisema endapo akikaa kwa muda mrefu sana ni dalili za mtu kuanzisha ufalme wake kama ilivyo kwa marais wa Afrika akitoka madarakani anamuacha mtoto wake.
“Hii inaonyesha kama mtu akikaa kwa muda mrefu sana inaanza kutokea kwa dalili za mtu kuanzisha ufalme tumeona kwa marais wengine wa Afrika wanakaa muda mrefu akitoka anamuacha mtoto wake ili kuepusha hili tuwe na demokrasia,” alisema
Aliongezea kuwa “Kuna watu kwa sababu zao binafsi wanataka abaki alipoingia Rais Hassan Mwinyi walisema abaki, alipoingia Benjamin Mkapa kuna watu walisema abaki, alipoingia Jakaya Kikwete wakasema hivyo hivyo na John Magufuli akasema hapana. Mara nyingi ni watu ambao wana maslahi yao wanaona huyu akiwepo maslahi yao yatakwenda vizuri tufuate demokrasia miaka 10 sio michache,” alisema Jaji Warioba.
SOMA HABARI HIZI KIRAHISI KUPITIA APP YETU YA UDAKU SPECIAL
Aidha, alisema kuna baadhi ya viongozi wanashindwa kuheshimu tunu za taifa ambazo ndio misingi ya uongozi na kushindwa kuheshimu nafasi wanazotumikia wananchi kwa mujibu wa katiba.
“Haya ndio mambo yanatuletea matatizo makubwa katika uongozi unakuta viongozi wasio na nidhamu, uadilifu, maadili na hawafuati misingi ya uongozi na wengine wanatumia madaraka yao vibaya lazima yawemo katika katiba na kuweka miiko ambayo inaelekeza viongozi wasifanye hivi na vile,” alisema Jaji Warioba.