Waziri Kabudi Akanusha Kuwafukuza Wamarekani na Kuwarudisha Watanzania Nchini...
0
February 02, 2020
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Prof. Palamagamba Kabudi, amekanusha kuwa taarifa zinazosambaa mitandaoni zikimnukuu kuwa amedai atawarudisha Watanzania nchini na kuwazuia raia wa Marekani wanaotaka kuingia nchini Tanzania kufuatia hatua ya nchi hiyo kumzuia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuingia nchini humo kwa madai ya kukiuka haki za binadamu.
Taarifa moja inayosambaa kwa kasi mitandaoni imemnukuu Waziri Kabudi akitishia kuwarudisha raia wa Tanzania nchini na kuweka vikwazo kwa raia wa Marekani wanaotaka kuingia nchini ikiwa ni njia ya kujibu hatua iliyochukuliwa na Taifa hilo la Magharibi dhidi ya Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda.
"Tunafanya mawasiliano na Balozi wa Marekani ili watueleze kwanini wametoa katazo kama hili....Ikishindikana tutawarudisha raia wetu na wao tutawazuia pia,"
Akizungumza na Mratibu wa Mtandao wa Watetezi Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, ambaye aliwasiliana nae na kutaka kujua ukweli wa taarifa hiyo, Waziri Kabudi amesema kuwa taarifa hiyo ni uzushi wala haina ukweli wowote.
Prof. Kabudi amesisitiza kuwa yeye ni mtu mwelewa, ambaye anafahamu taratibu zote za kidiplomasia, hivyo hawezi kutoa kauli kama hiyo.
"Ninaomba Watanzania kuzipuuza taarifa hizo. Mimi ni muelewa na ninafahamu vizuri taratibu za kidiplomasia. Siwezi kutoa kauli kama hiyo," ameeleza Prof. Kabudi ambaye pia ni mwanataaluma mkubwa nchini aliyebobea katika masuala ya sheria.
Kunukuliwa kwa kauli hiyo ambayo Prof. Kabudi amedai kuwa sio yake, kumekuja kipindi cha takribani siku moja kufuatia taarifa ya kumpiga marufu kuingia nchini Marekani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na mkewe Mary Massenge, kutokana na madai ya kile kinachoelezwa kuwa Mkuu huyo wa Mkoa amekuwa akishiriki katika ukandamizaji wa haki za binaadamu ikiwemo haki ya kuishi, haki ya uhuru wa kujiamulia mambo na usalama wa watu.
Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Michael Pompeo Januari 31, 2020 aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa Makonda amekuwa akishiriki kwa kiasi kikubwa katika ukiukaji wa haki za binadamu, ambapo ameeleza pia wasiwasi wake kuhusu kuporomoka kwa hali ya haki za binadamu nchini Tanzania.
"Leo tumetangaza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Christian Makonda kuwa hataruhusiwa kuingia Marekani kwa kushiriki kwake katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu. Tuna wasiwasi mkubwa juu ya kuporomoka kwa heshima ya haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania," aliandika Pompeo.
Hatua ya kuzuiliwa kwa Makonda kuingia nchini Marekani ilipongezwa pia na Bunge la Senate nchini Marekani, ambapo limedai kuwa hatua hiyo ya mwanzo ni nzuri, kwani inalenga kuwawajibisha wale wote wanaozorotesha demokrasia.
Hata hivyo, baadae tena serikali ya Marekani ilitangaza kupiga marufuku raia wa Tanzania kushiriki bahati nasibu ya kupata viza ya kuingia Marekani.
Bahati nasibu hiyo hutoa viza takribani 50,000 kwa raia wanaotoka katika nchi zenye kasi ndogo ya maendeleo kila mwaka kuingia na kufanya kazi Marekani.
Tags