Yanga Hii Mtateseka Sana
0
February 04, 2020
YANGA imeshashika kasi yake. Kama ni gari tayari limeshakoleza moto na kwa mwendo huu, wapinzani wao watateseka sana.
Yanga juzi imeshinda tena baada ya kuichapa timu ngumu ya Mtibwa Sugar bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Hiyo ni mechi ya tatu mfululizo Yanga inashinda ikiwa chini ya kocha mpya, Mbelgiji, Luc Eymael baada ya kupoteza mechi zake mbili za kwanza dhidi ya Kagera Sugar na Azam tangu akabidhiwe rasmi mikoba ya kumrithi Mcongo, Mwinyi Zahera.
Bao pekee la Yanga lilifungwa na David Molinga aliyemchambua kipa wa Mtibwa Sugar, Shaaban Kado akipokea krosi safi ya Nchimbi.
Dakika 15 baada ya kufunga, Molinga alipiga shuti jingine kali lililogonga mwamba wa juu na kurudi uwanjani, kisha kipa akadaka.
Dakika ya 72, Riphat Msuya wa Mtibwa alikosa bao la wazi akiwa amebaki yeye na kipa.
Yanga waliuanza mchezo huo kwa kasi wakilisakama lango la Mtibwa. Dakika ya pili tu, Patrick Sibomana alikuwa ameshatikisa nyavu kwa shuti kali ndani ya eneo la hatari lakini mwamuzi akalikataa bao hilo akidai ni offside.
Lakini hadi mapumziko mpira huo ulionekana kuwa ni 50/50 huku kiungo mwenye mbwembwe Yanga, Bernard Morrison, akishindwa kufurukuta katika kipindi cha kwanza.
Yanga wangeweza kupata bao la kuongoza dakika ya 36 wakati beki Lamine Moro alipopiga shuti lililogonga mwamba kisha mpira ukadakwa na kipa mkongwe wa Mtibwa, Shaaban Kado. Moro alikuwa akiunganisha mpira wa faulo uliopigwa na Morrison.
Katika mchezo huo, inaonekana Mtibwa walijua ubora wa Morrison, hivyo walikuwa wakimchezea rafu za mara kwa mara. Hadi anakwenda mapumziko, alikuwa ameshachezewa rafu sita.
Hata hivyo, kipindi cha kwanza Morrison alikuwa amepiga pasi 11 zilizofika na nne zisizo sahihi. Alikuwa amekokota mpira mara tano ndani ya kipindi hicho, akipiga kona mbili, krosi mbili na kuotea mara moja.
Kwa upande wa kiungo mwingine fundi wa Yanga, Haruna Niyonzima, kipindi cha kwanza alipiga pasi za uhakika 27, pasi iliyokufa ikiwa ni moja, alikokota mpira mara sita, alicheza faulo mbili na alichezewa faulo moja na kupiga kona moja.
Dakika ya 45, Yanga walimtoa Sibomana na kumuingiza Ditram Nchimbi ambaye mabadiliko yake yalizaa matunda kwani dakika tano baadaye alitoa pasi ya bao lililofungwa na Molinga.
Morrison alitoka dakika ya 85 na kuingia Abdulaziz Makame. Wakati akitoka alipigiwa makofi na mashabiki wa Yanga licha ya kuwa hakuwa kwenye ubora kama wa mechi mbili zilizopita.
Sasa Yanga imepanda hadi nafasi ya nne ikiwa na pointi 31, sawa na Namungo iliyo nafasi ya tatu lakini Yanga ikizidiwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Sasa Yanga imebakiza pointi 16 iwafikie vinara Simba kileleni lakini Yanga wakiwa na viporo viwili.
Kikosi cha Yanga kilichoanza ni: Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffar Mohammed, Lamine Moro, Juma Makapu, Papy Tshishimbi, Patrick Sibomana, Haruna Niyonzima, David Molinga/ Yikpe Gnamien dk ya 68, Mapinduzi Balama na Bernard Morrison.
Mtibwa: Shaaban Kado, Kibwana Shomari, Issa Rashid, Cassian Ponela, Henry Shindika, Abdulhalim Mohamed, Ismail Mhesa/Juma Luizio dk 66, Ally yusuph, Riphat Msuya, Awadha Juma na Salum kihimbwa.
WILBERT MOLANDI NA MARCO MZUMBE, Dar
Tags