Zitto: Sio kosa kuiandikia barua Benki ya Dunia isiipe mkopo Tanzania


Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania, Zitto Kabwe amesema haoni kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali atamkuta na kosa kutokana na kuiandikia barua Benki ya Dunia (WB) akitaka isiidhinishe mkopo wa Sh1.2 trilioni kwa Tanzania kwa ajili ya sekta ya elimu.

Zitto ameeleza hayo leo Jumanne Februari 18, 2020 katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu ya kutetea nafasi yake katika uchaguzi wa chama hicho.

Katika mkutano wa 18 wa Bunge uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, Zitto alishukiwa na wabunge kwa kitendo chake hicho huku Spika Job Ndugai akisema watamsubiri arejee nchini ili wamuulize sababu za kufanya hivyo, hapohapo akamtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuangalia kama kuna uwezekano wa kuwemo jinai katika kitendo hicho.

Katika mkutano wake huo Zitto amesema, “sioni kosa lolote ambalo Mwanasheria Mkuu wa Serikali anaweza akalikuta kwamba nimelifanya kwa kuandika barua WB. Hizi ni siasa tu ambazo zilikuwa hazifanyiki huko nyuma, au watu walikuwa wanafanya kwa kificho sasa mimi nimezifanya kwa uwazi ndio tofauti tu hiyo, haina maana kuwa ni kitu kipya sana”

Amesema kila Mtanzania ana haki ya kuwasiliana na Benki ya Dunia iwapo Serikali yake kuna mambo imekosea katika maombi ya fedha katika benki hiyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad