Zitto Kabwe: Siogopi Kubambikiziwa Uhujumu Uchumi, Utakatishaji Fedha (USD 2M), Nakuja!
0
February 15, 2020
Leo Februari 14, 2020 Kiongozi wa Chama cha ACT wazalendo, Ndugu Zitto Kabwe, ambaye yupo nje ya nchi katika harakati za kuhami Demokrasia yetu ya Tanzania kwa kuhamasisha mshikamano na Jumuiya za Kimataifa, ameandika yafuatayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter;
Aprili 2019 nilihoji Bungeni “TAKUKURU ndio taasisi ambayo tumeipa dhamana ya kupambana na rushwa, Bajeti ya 2019/2020 tunawaombea Sh 75 bilioni LAKINI hesabu zake hazijawahi kukaguliwa na mkaguzi yeyote yule.” Ni kwanini hawakaguliwi wala hawafungi hesabu?
Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inataka Taasisi ya TAKUKURU kukaguliwa mahesabu yake. Lakini kwa kujificha mgongo wa Ofisi ya Rais ambayo Bajeti ya Taasisi hii hupitishwa, TAKUKURU wanakwepa Ukaguzi. Prof. Assad alipotaka kuikagua alizuiwa na Rais. Kwanini?
Ni kwa sababu TAKUKURU inatumika kisiasa. Kama ilivyo Ofisi ya DPP na kwa kushirikiana, TAKUKURU hutumiwa na Dola kusumbua, kutisha au kubambikia watu Kesi iwapo wanakwenda kinyume na watawala. Wanasiasa wa CCM wanaopingana na utawala wa Magufuli na wa upinzani wakosoaji hulengwa.
Mwezi Machi mwaka 2017 niliitwa na TAKUKURU kuhojiwa kuhusu kilichoitwa kupokea Fedha kutoka Benki ya Standard Chartered Hong Kong ili kuwasaidia katika uchunguzi wa uporaji wa Fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
Nilipowauliza TAKUKURU nani kawaeleza upuuzi huo wakasema kuwa wameletewa barua na Mbunge mmoja wa zamani ( hivi sasa ni RAS ). Nikawaambia Mbunge huyo kawadanganya na mlipaswa kujiridhisha kwanza kwani Standard Chartered ni Benki kubwa na haiwezi kujiingiza kwenye upuuzi.
Niliomba kumwona Bwana Mlowola Wakati huo akiwa Mkuu wa Taasisi na kumwambia uso kwa uso kuwa taasisi yake inatumika kisiasa. Narudia kumwambia Kaimu Mkurugenzi wa sasa hadharani kuwa taasisi yake inatumika kisiasa na yeye kakubali kutumika.
Baada ya kuwaelimisha namna uchunguzi wa Tegeta Escrow ulivyofanywa na kuwaambia wawakamate waliochota Fedha Benki Kuu na kwamba nilifanya kazi yangu pamoja na wajumbe wa PAC kwa weledi wa hali ya juu sana, hawakuniita tena kuhusu hilo.
Mwaka 2018 wakaniita kuhusu tuhuma nilizowapa Watendaji wa Serikali kuhujumu Mradi wa Mchuchuma na Liganga. Nikawapa maelezo yangu ya kutosha. Ulikuwa usumbufu maana hawajachukua hatua yoyote dhidi ya wahujumu ambao ni pamoja na Rais Magufuli.
Sasa TAKUKURU wanarudi tena kwenye Tegeta Escrow kwa tuhuma zingine za kubumba zenye lengo la kuniweka ndani muda mrefu ili nisishiriki Uchaguzi Mkuu. Ninawaambia tena, SIOGOPI. TAKUKURU Waache kufanya kazi kama Jumuiya ya Nne ya CCM - Wazazi, Wanawake, Vijana na TAKUKURU.
" I Want to be very clear to PCCB (TAKUKURU) that I am ready for their bogus USD 2 million money laundering and organized crimes charges against me. Target is to block me from 2020 elections. I know that. Let us see."
Ndugu Zitto anamalizia kwa kusema;
"Wala wasidhani kuwa nitaogopa kurudi Tanzania. Nitarudi mchana kweupe. Nitakuwa Mahakamani kusikiliza hukumu ndogo ya Kesi yangu ya uchochezi na pia kesi yangu dhidi ya Rais Magufuli kuvunja katiba ya nchi kwa kumfuta kazi CAG. Zote siku ya Jumanne tarehe 18/2/2020."
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akiambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya fedha Nassor Mazrui amefanikiwa kufanya ziara katika nchi za Uingereza, Canada na Marekani. Ndugu Zitto hakuweza kuhudhuria kesi ya Uchochezi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Februari 10, 2020 kutokana na changamoto za kiafya.
Suphian Juma,
Afisa Habari, ACT wazalendo.
Februari 14, 2020.
Source: Jamii Forums
Tags