Rais Magufuli amesema watu 12 wamebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona nchini Tanzania.
Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la wagonjwa sita kutokana na kuwepo wengine sita hadi leo asubuhi Jumapili Machi 22, 2020 kabla ya Rais Magufuli kutoa tamko hilo leo mchana.
Katika hotuba yake kwa Taifa , Rais Magufuli amebainisha kuwa kuanzia kesho wasafiri watakaoingia Tanzania kutoka nchi zenye maambukizi ya corona watawekwa katika eneo maalum kwa siku 14 kwa gharama zao wenyewe.
“Mpaka sasa nchi yetu imebaini wagonjwa 12 ambao wamethibitika kuambukizwa corona. Kati yao wanne ni raia wa nje na wanane ni raia wa Tanzania. Wagonjwa wote isipokuwa mmoja ametoka kwenye nchi zilizokuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
“Wagonjwa wote wanaendelea vizuri na hadi sasa hakuna kifo kinachotokana na corona. Vipimo vya leo vyote vilivyochukuliwa hakuna aliyekutwa na maambukizi, vilikuwa vipimo vya watu 20. Hata mgonjwa wetu wa kwanza kupata ugonjwa huu kule Arusha ameonekana hana tena ugonjwa,” amesema Magufuli.
Akizungumzia hatua mpya zilizochukuliwa Magufuli amesema, “Kuanzia kesho Machi 23 wasafiri wote watakaoingia nchini kutoka kwenye mataifa yaliyoathirika zaidi na ugonjwa huu watalazimika kufikia sehemu zilizotengwa na kukaa huko kwa siku 14 kwa gharama zao wenyewe.
“Maelezo haya yatawahusu pia Watanzania wanaotoka katika nchi hizo ambao walikwenda kwa shughuli mbalimbali. Naelekeza Wizara ya Afya na Mamlaka nyingine husika kuimarisha maabara ya Taifa na kuipatia vifaa vya kisasa.
“Tumeamua kuimarisha kamati ya kitaifa ya kukabiliana na ugonjwa huu ambayo itakuwa chini ya Waziri mkuu akisaidiwa na waziri wa Afya. Wajumbe wengine watachaguliwa na Waziri Mkuu kulingana na umuhimu wao.”