Afrika Kusini imekuwa nchi ya hivi punde ya chini ya jangwa la Sahara barani Afrika kuthibitisha kuwa na mtu anayeugua homa inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).
Akizungumza masaa machache baada ya kuthibitishwa kesi hiyo ya kwanza ya Corona nchini Afrika Kusini, Rais Cyril Ramaphosa wa nchi hiyo amesema kuingia kwa ugonjwa huo hatari kutakuwa na taathira hasi kwa sekta ya utalii na uchumi wa nchi hiyo ambao tayari unayumba.
Ameongeza kuwa, "tutazidi kuwataarifu Waafrika Kusini kwa uwazi kuhusu hatua tulizochukua, kwa kuwa kesi hii huenda ikageuka na kuwa mgogoro wa kitaifa."
Awali, Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Zweli Mkhize aliliambia Bunge kuwa, aliyekumbwa na Corona ni mwaume wa miaka 38, aliyekuwa amesafiri kwenda Italia pamoja na mkewe na kisha kurejea nchini humo wakiwa pamoja na watu wengine 10 mnamo Machi Mosi. Waziri huyo ameongeza kuwa, tayari watu hao wamewekwa katika karantini ili kuzuia maambukizi zaidi.
Kabla ya Afrika Kusini, nchi nyingine za Afrika ambazo zimethibitisha kuwa na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona ni Algeria, Misri, Morocco, Nigeria, Senegal na Tunisia.