DEREVA wa basi la Isamilo lenye namba za usajili T609 CQB aina ya Scania linalofanya safari zake kati ya Mwanza na Mbeya, Sebastian Mathias (43) mkazi wa Mwanza, amefariki dunia wakati akiwa safarini na basi lake kutoka Mbeya kwenda Mwanza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Deborah Magiligimba, amesema tukio hilo limetokea leo Ijumaa, Machi 20,2020 majira ya saa nne asubuhi eneo la Tinde mkoani Shinyanga.
“Sebastian alitoka Mwanza kwenda Mbeya akiwa anajisikia vibaya, huwa wapo madereva wawili wanaokwenda hadi Mbeya. Wakati wakitoka Mbeya kurejea Mwanza aliendelea kujisikia vibaya, walipofika Singida akajisikia vibaya zaidi ndipo akampa dereva mwenzake kuendesha.
“Lakini walipofika Tinde majira ya saa nne asubuhi, akawa amezidiwa sana, wenzake walimbeba na kumpeleka katika Kituo cha Afya Tinde, na baada ya kumfikisha, daktari alimpima akabaini kuwa tayari Sebastian alikuwa amefariki dunia,” amesema na kuongeza kwamba dereva mwingine ameendelea na safari kwenda Mwanza.