Siku zote katika maisha yako kabla hujatenda kitu chochote, kabla hujasema kitu chochote, jiulize kitu unachotaka kutenda au kitu unachotaka kusema je, kitaleta matokeo chanya kwako au hata kwa wengine?
Sio kwa sababu unayo nafasi nzuri ya kutenda au kusema hiyo ikawa na maana kwako ufanye au useme tu hata mambo yanayoumiza wengine. Unatakiwa kuwa makini na kuzingatia ni nini matokea ya kile ambacho unakwenda kutenda au kukizungumza. Kwani kila wakati tunakumbushwa ya kwamba ni heri kufikiri kabla ya kutenda.
Nisisitiza suala la kufikiri kabla ya kutenda kwa sababu wengi wetu hukurupuka katika kutenda mambo fulani, na kufanya hivyo kumekuwa chanzo cha kutotimiza jambo hilo. Hivyo kwa jambo lolote kabla ya kulitenda au kulisema ni heri kulitakari mara dufu zaidi.
Pia kufikiri kabla ya kutenda ni muhimu kwa sababu ni dhahiri wapo watu ambao moja kwa moja utawaumiza, kama utatenda au kusema maneno hasi, hata kama hujui jinsi unavyowaumiza. Pia uelewe wapo watu utakaowaponya kama utaamua kusema au kutenda matendo chanya ambayo yana msaada mkubwa katika maisha yao kwa ujumla.
Kila wakati, unayo nafasi nzuri sana ya kutoa mazuri katika dunia, ingawa uamuzi ni wako. Acha kutenda au kusema mara moja kile kinachokujia kichwani mwako, Jipe muda wa kukifikiri kitu hicho na kujua ni nini matokeo yake katika maisha yako na ya wengine.
Kuanzia leo jifunze kutoa yale mazuri katika hii dunia jenga utamaduni wa kutoa yale matendo au maneno mazuri iwe sehemu ya utamaduni wako. Ukifanya hivyo dunia itakupa mazuri pia na utafurahia maisha yako kutokana na mazuri unayoyatoa.
Simama imara katika kuhakikisha unalitenda hili vyema kila wakati. Simamia katika ukweli, ili kutengeneza amani ya moyo wako na mioyo ya watu wengine. Usiwe kichocheo katika kusababisha watu wengine wakose furaha, bali jitahidi kuwa katika kusimamia ukweli na haki daima.
Kumbuka sana TOA YALE MAZURI KATIKA MAISHA YAKO, GIVE GOODNESS TO LIFE, ukifanikisha hili furaha na mafanikio vitakuwa upande wako.
Mwisho tuweke nukta kwa kusema ya kwamba wewe ni matokeo ya mafanikio ya watu wengine kama utaamua kuwa mkweli kwa kutakari kabla ya kusema na kutenda utafanya vichocheo vya mafanikio kwa watu wengine.
Imeandaliwa na mtandao wa dira ya mafanikio,
Imani Ngwangwalu & Benson Chonya,