Dar es Salaam. Beki wa Kimataifa wa Tanzania, Abdi Banda anayeichezea Highlands Park inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini 'PSL', amesema anaendelea vizuri licha ya kuchukuliwa vipimo vya ugongwa wa virusi vya Corona.
Banda ambaye alijihisi kuwa na dalili za Corona alisema hakuna na namna zaidi ya kufanyiwa vipimo kwa lengo la kufahamu afya yake na mara baada ya zoezi hilo kukamilika alipewa ruhusa ya kwenda kupumzika nyumbani.
"Naendelea vizuri lakini ni vyema kusubiri majibu. Niliongea na viongozi na kuwaeleza naendelea poa na majibu wakanieleza kuwa huenda yakatoka kesho," alisema Banda.
Beki huyo wa zamani wa Simba na Coastal Union za Ligi Kuu Tanzania Bara, hakuwa sehemu ya kikosi cha Highlands siku mbili zilizopita ambacho kilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Mamelod Sundowns 'Masandawana' katika kombe la Nedbank.
Aliichezea klabu yake kwa mara ya mwisho katika mchezo wa Ligi Kuu Afrika Kusini 'PSL' Machi 8 ambapo walipoteza wakiwa nyumbani kwa mabao 2-0 dhidi ya Supersport United.
Afrika Kusini ni miongoni mwa mataifa ya Afrika ambayo yamebainikia kuwa na wagonjwa wenye virusi hivyo ambavyo vimetangazwa kuwa kwa sasa vimeenea duniani kote.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, Dk Tedros Ghebreyesus ametangaza akiwa mjini Geneva, Uswisi hii leo.
Dk Tedros alisema kuna zaidi ya wagonjwa 118,000 katika mataifa 114 ambapo tayari watu 4,291 wamefariki dunia.
“Maelfu wengine wako taabani hospitali wakihaha kuokoa maisha yao. Katika siku na wiki zijazo, tunatarajia kuwa idadi ya wagonjwa itaongezeka, sambamba na idadi ya vifo na idadi ya nchi yenye wagonjwa halikadhalika.
"WHO imekuwa ikitathmini mlipuko na tumekuwa na hofu kubwa ya kuenea kwa ugonjwa huu na vile vile ukosefu wa uchukuaji hatua,” alisema Dk Tedros.